12. Kutotaja kauli kinzani mbele ya Mwanazuoni na katazo la kuchukuwa ruhusa za Wanazuoni (katika waliyokosea)


Wapo baadhi ya watu wanawauliza Wanazuoni kwa njia za simu, na simu siku hizi zimekithirisha matatizo ya maswali.
Utakuta anamuuliza Mwanazuoni mmoja kisha baada yake anamuuliza wapili,watatu na wanne, utakuta anajichanganya kwenye suala (fulani), kisha baada ya hayo utamuona anapita njia isiyo nzuri.
Anapita katika njia ya kuifanyia kazi ile fat’wa ambayo kwake ni rahisi zaidi kuliko nyengine.
Na uulizaji wa maswali kwa njia hii haufai. Njia inayofaa ni wewe kumtafuta unayemuamini kwa Dini yake na elimu aliyonayo kisha ukamuuliza , kama walivyosema Wanazuoni (wetu):
“ينبغي للمستفتي أن يسأل من يثق بعلمه ودينه”
“Inampasa muuliza fa’twa amuulize yule anayemuamini kwa elimu yake na Dini”.
Hivyo utakapokuwa umemuamini fulani (katika ‘Ulamaa) kwa elimu yake na Dini yake basi muulize na wala usimuulize mwengine. Kwasababu kama utamuuliza mwengine huwenda akawa na jawabu kinyume na lile la kwanza mwishowe ukabaki katika njia panda hujui cha kufanya.
بتصرف
faida
Kuwauliza masheikh wengi suala moja ni katika mambo yaliyokemewa sana na Wanazuoni mbaya zaidi ni muulizaji awe na dhamira ya kupata fat’wa yenye unafuu kwake.
Pamoja yakuwa huenda ile fat’wa nyepesi kwake ikawa imesibu zaidi kuliko nyengine, au ikawa imekosewa zaidi kuliko nyengine, na njia kama hii mara nyingi humpelekea mtu kubaya , akawa na tabia ya kutafuta mtelezo wa Wanazuoni (تتبع الرخص) ili kujihalalishia mambo yake. Na bila shaka dhamira mbovu kama hizi zimekemewa vikali katika Shari’ah.
Imepokelewa khabari katika kitabu “siyar a’laam al-nubalaa” (13/465) katika tarjamah ya Al-Mu’tadhid Billah. Kwamba Ismaa’il Al-Qaadhiy aliingia siku moja kwa Khalifa Mu’tadhid Billaah, akampa kitabu, Al-Qaadhiy akakisoma kile kitabu, tahamaki ndani ya kitabu kile kumekusanywa fatawa zilizotokomana na kukosea kwa Wanazuoni (kuteleza). Akasema (Al-Qaadhiy):
Muandishi wa hiki kitabu ni mtu mzandiki.
Akauliza Al-Mu’tadhi:
Kwani hadithi zake hazijaswihi!?
Akasema Al-Qaadhiy:
Ni kweli kwamba hadithi zipo ila aliyehalalisha (katika Wanazuoni) vilevi hakuhalalisha ndoa ya mut’ah, na aliyehalalisha mut’ah hakuhalalisha nyimbo, na wala hakuna ‘Aalim yeyote ila anateleza, na atakayebeba mitelezo ya Wanazuoni itapotea Dini yake. Kisha akaamrisha kitabu kichomwe moto”.
Muhusika: Shaykh Swaalih Aalish-Shaykh
Mtarjimu: duaatsalaftz.net
Marejeo: adabus-suaal uk.19
Imehaririwa: 24’jumaadal-uwlaa/1438H