13. Thawabu kwa mwenyekulazimiana na msikiti na akaketi humo kwa jambo la kheri


Amesema Allaah Mtukufu:
“Hakika si vinginevyo wenyekuimarisha misikiti ya Allaah na wale wanaomwamini Allaah na siku ya mwisho, na wakasimamisha swala na kutoa zaka na hawamuogopi yeyote isipokuwa Allaah, kwa hakika hao watakuwa ni miongoni mwa walioongoka”. [al-tawbah 18].
Na amesema Allaah Mtukufu:
“Katika nyumba (za Allaah) , ametoa idhini Allaah zijengwe na litajwe humo jina lake (na kusomwa kitabu chake), wanamsabihi humo asubuhi na jioni wanaume ambao hawapumbazwi na biashara wala kuuza na kununua kutokana na kumdhukuru Allaah na kusimamisha swala na kutoa zaka, wanaogopa siku ambayo nyoyo na macho yatageuka.
Ili Allaah awalipe kwa mazuri waliyoyafanya na kuwazidishia katika fadhila zake, na Allaah humruzuku amtakaye pasi na hesabu”. [al-nuur 36-38].
Imepokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah (Allaah amridhie) amesema,
“Nimemsikia Mtume wa Allaah (swalla Llaahu ‘alayhi wasallam) akisema:
“Watu wa aina saba atawaweka Allaah kwenye kivuli chake siku ambayo hakutokuwa na kivuli zaidi ya kivuli chake:
1. Kiongozi muadilifu
2. Kijana aliyekulia kwenye makuzi ya ibada za Allaah -‘azza wajalla-
3. Mtu ambaye moyo wake umefungamana na misikiti
4. Na watu wawili waliopendana kwaajili ya Allaah na kufarikiana juu yake
5. Na mtu aliyetakiwa (kwa machafu) na mwanamke mwenye nafasi (nzuri) na mrembo, akasema namuogopa Allaah -‘azza wajalla-
6. Na mtu aliyetoa sadaka kwa kificho mpaka ukashindwa kujua mkono wake wa kushoto kilichotolewa na mkono wake wa kulia
7. Na mtu aliyemdhukuru Allaah katika hali ya upweke (faragha) kisha yakabugujika machozi macho yake”.
Sahihi: ameipokea Bukhary (660), na Muslim (1031).

Muhusika: Ikhtiyaar ‘Ubayd
Mtarjimu: duaatsalaftz.net
Marejeo: miiraathun-Nabiyy uk.6
Imehaririwa: 4’jumaadal-uwlaa/1438H