23.Faida Katika Hadeeth ya Jibriyl-18


Aliposema: Ewe Muhammad! Nikhabarishe kuhusiana na Uislam.
Akasema Mtume wa Allāh (swalla Llāhu’alayhi wasallam):
“Uislam ni kushahadia kuwa hakuna Mola apasayekuabudiwa kwa haki isipokuwa Allāh, na kwamba Muhammad ni Mtume wa Allāh, na usimamishe swala, na utoe zaka, na ufunge mwezi wa Ramadhani, na uhiji katika Nyumba ya Allāh kama una uwezo wa kufika huko”.
Akasema: Umesema kweli.
Anasema (Umar): Tukamstaajabu anamuuliza huku akimsadikisha.
Katika maelezo haya kuna faida nyingi:

Ya kwanza:

Mtume (swalla Llāhu’alayhi wasallam) amemjibu Jibriil kwa yale mambo ya dhahiri pale alimuuliza kuhusu Uislam, na amemjibu kwa mambo ya ndani (yaliyofichikana) pale alipomuuliza kuhusu Iymān.
Na neno Islām na Iymān yanapojumuishwa katika utajo hufarakanishwa katika maana.
Na hapa yametajwa kwa pamoja, hivyo likatafsiriwa neno Islām kwa yale mambo ya dhahiri ambayo yananasibiana kabisa na uhalisia wa Uislām, ambao ni kunyenyekea kwa Allāh, na Iikatafsiriwa neno Iymān kwa mambo ya ndani (ya moyo), nayo ni tafsiri inayonasibiana kabisa na uhalisia wake, ambao ni kusadikisha na kukubali.
Na pindi litajwapo kila moja kwa upweke basi hubeba pia maana ya jengine, kwa maana hubeba maana ya yale yote yaliyofichikana na yaliyodhahiri.
Na mfano wa kuja kwa neno Islām peke yake, ni kauli ya Allāh ‘-Azza wajalla-:

وَمَن يَبْتَغِ غَيْرَ الْإِسْلَامِ دِينًا فَلَن يُقْبَلَ مِنْهُ وَهُوَ فِي الْآخِرَةِ مِنَ الْخَاسِرِينَ        ” آل عمران (85)

“Na yeyote atakayetaka Dini isiyokuwa ya Kiislamu, halitokubaliwa hilo kutoka kwake, na yeye siku ya mwisho atakuwa ni miongoni mwa waliokula hasara”
Al-Imran (85).
Na mfano wa kuja neno Iymān peke yake, ni kauli ya Allāh ‘-Azza wajalla-:

“وَمَن يَكْفُرْ بِالْإِيمَانِ فَقَدْ حَبِطَ عَمَلُهُ وَهُوَ فِي الْآخِرَةِ مِنَ الْخَاسِرِينَ      ” المائدة (5)

“Na yeyote atakayeikana Iymān basi kwa hakika zimeanguka amali zake, na yeye siku ya mwisho atakuwa ni miongoni mwa waliokula hasara”.
Al-Maida (5).
Na mfano wa hilo, ni neno fakiri na masikini, birri, na taq-wa, na mengineyo.[1]
————————–
[1] Akiwa ana maana ya kuwa ukiona neno maskini limetajwa peke yake fahamu kuwa fakiri naye yumo humo.

 

Muhusika: Shaykh ‘Abdul-Muhsin Al-‘Abbād Al-Badr
Mtarjim: http://duaatsalaftz.net/
Marejeo: Sharh Hadith Jibriil