23. Thawabu za tahajjud na qiyaamul-layl


Imepokelewa kutoka kwa Abuu Sa’iid na Abuu Hurayrah (Allaah awaridhie), wamesema:
Amesema Mtume wa Allaah (swalla Llaahu ‘alayhi wasallam):
“Yeyote atakayeamka wakati wa usiku na akamuamsha mkewe wakaswali kwa pamoja rakaa mbili (tu), wataandikwa kuwa ni miongoni mwa wamdhukuruo Allaah kwa wingi katika wanaume na wanawake”.
Sahihi: ameipokea Abuu Daud , na ameifanyia takhriij Al-Albaaniy katika sahihi ya Abiy Daud (1181), na Al-Nasaiy katika “al-kubraa” kama yalivyokuja maelezo katika “tuhfatul-ash-raaf” (3/331), na ibn Maajah (1335), na ibn Hibban (2560), na Al-Haakim (1/316).
Imepokelewa kutoka kwa ‘Abdullaah bin Mas’uud (Allaah amridhie), amesema:
Amesema Mtume wa Allaah (swalla Llaahu ‘alayhi wasallam):
“Hakuna kuhusudiana ila kwenye mambo mawili:
1. Ni mtu aliyepewa na Allaah mali, akawa anatoa sehemu ya mali yake nyakati za usiku na mchana.
2. Na mtu aliyepewa na Allaah (kisomo) cha Qur-aan akawa anasimama (kuswali) nyakati za usiku na mchana”.
Sahihi: ameipokea Muslim (815), kutoka kwa ‘Abdillaah bin ‘Umar.
Tanbiih
Hasadi ni haramu na ni katika madhambi makubwa kabisa.
Kusudio la hasadi katika hiyo hadithi kama wasemavyo Wanazuoni ni ghibtwah ambayo maana yake ni kutamani neema aliyonayo mwenzako pasi na kutamani imuondoke.
Sasa kanakwamba Mtume (swalla Llaahu ‘alayhi wasallam) anatuambia, kama kuna mambo yaliyoruhusika mtu kumuonea wivu wa kheri nduguye (pasi na kutamani aharibikiwe) ni yule aliyepewa mali akawa anazitumia kwenye njia za kheri na utiifu.
Na aliyepewa elimu ya dini (kama ilivyokuja katika baadhi ya mapokezi), akawa anawafunza watu na akawa anaitumia usiku na mchana.
Muhusika: Ikhtiyaar ‘Ubayd
Mtarjimu: duaatsalaftz.net
Marejeo: miiraathun-Nabiyy uk.8-9
Imehaririwa: 6’jumaadal-uwlaa/1438H