25. Thawabu za kuswali swala ya ijumaa na fadhila za siku yake na muda wake


Imepokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah (Allaah amridhie), kutoka kwa Mtume wa Allaah (swalla Llaahu ‘alayhi wasallam) amesema:
“Swala tano, na ijumaa mpaka ijumaa, na ramadhani mpaka ramadhani, ni vifutio (vya madhambi) yaliyo baina yake pale yatakapoepukwa madhambi makubwa”.
Sahihi: ameipokea Muslim (233).
Imepokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah (Allaah amridhie), amesema:
Amesema Mtume wa Allaah (swalla Llaahu ‘alayhi wasallam):
“Yeyote atakayeshika udhu vyema, kisha akaiendea (swala) ya ijumaa , akasikiliza kwa makini na kunyamaza kimya, atasamehewa (madhambi) baina ya ijumaa hiyo na iliyopita, na ziada ya siku tatu”.
Sahihi: ameipokea Muslim (857).
Imepokelewa kutoka kwa Abuu Sa’iid Al-Khudriy (Allaah amridhie), kwamba hakika amemsikia Mtume wa Allaah (swalla Llaahu ‘alayhi wasallam), akisema:
“Mambo matano akiyatenda mtu kwa siku, Allaah atamuandika katika watu wa peponi:
1. Atakayemtembelea mgonjwa
2. Na akahudhuria swala ya jeneza
3. Na akafunga siku moja
4. Na akarauka (akadamka) mapema kuindea ijumaa
5. Na akaacha mtumwa huru”.
Sahihi: ameipokea ibn Hibban (2760), na ameisahihisha Al-Albaaniy katika “sahiih al-targhiib” (686).
Na imepokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah (Allaah amridhie), kwamba hakika Mtume wa Allaah (swalla Llaahu ‘alayhi wasallam), aliitaja siku ya ijumaa, akasema:
“Ndani yake kuna muda hatouafiki mja Muislam ilhali amesimama akiwa anaswali akimuomba Allaah chochote ila hupewa”.
Sahihi: ameipokea Bukhary (935) na (852).
Na imepokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah (Allaah amridhie), amesema:
Amesema Mtume wa Allaah (swalla Llaahu ‘alayhi wasallam):
“Bora ya siku ambayo imechomozewa na jua, ni siku ya ijumaa.
Siku hiyo aliumbwa Aadam (‘alayhis-salaam), na siku hiyo aliingizwa peponi, na siku hiyo alitolewa”.
Sahihi: ameipokea Muslim (854).
Muhusika: Ikhtiyaar ‘Ubayd
Mtarjimu: duaatsalaftz.net
Marejeo: miiraathun-Nabiyy uk.9
Imehaririwa: 9’jumaadal-uwlaa/1438H