31. Thawabu za kutoa sadaka kwa siri


1. Imepokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah (Allaah amridhie) amesema:
Nimemsikia Mtume wa Allaah (swalla Llaahu ‘alayhi wasallam) akisema:
“Watu wa aina saba atawaweka Allaah kwenye kivuli chake siku ambayo hakuna kivuli chengine zaidi ya kivuli chake:
1. Kiongozi mwadilifu
2. Kijana aliyekuwa katika makuzi ya kumuabudu Allaah -‘azza wajalla-
3. Na mtu ambaye moyo wake umetundikwa misikitini (una mafungamano makubwa nayo)
4. Na wawili waliopendana kwa ajili ya Allaah na wakafarikiana juu yake
5. Na mtu ambaye ametakiwa na mwanamke mwenye nafasi na uzuri, akasema: hakika mimi namuogopa Allaah -‘azza wajalla-
6. Na mtu aliyetoa sadaka akaificha mpaka ukashindwa kujua mkono wake wa kushoto kilichotolewa na mkono wake wa kulia
7. Na mtu aliyemdhukuru Allaah kwa hali ya upweke kisha yakabugujisha machozi macho yake”.
Sahihi: ameipokea Bukhary (660) na Muslim (1031).
2. Imepokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah (Allaah amridhie), kutoka kwa Nabiy (swalla Llaahu ‘alayhi wasallam) amesema:
“Utajiri si kuwa na vitega uchumi vingi, lakini utajiri wa kweli ni utajiri wa kukinai nafsini”.
Sahihi: ameipokea Bukhary (6446), na Muslim (1051).
Tanbiih
Bila shaka sadaka ya siri ni bora zaidi kwasababu inamkurubisha mtu kunako ikhlasi kuliko sadaka ya dhahiri. Anasema Allaah:
(إن تبدوا الصدقات فنعماهي وإن تخفوها وتأتوها الفقراء فهو خير لكم) البقرة؛ ٢٧١
“Kama mtazidhihirisha sadaka basi ni jambo zuri hilo, na kama mtazificha na kuwapa mafakiri basi hilo ni bora zaidi kwenu”.
Na amesema ibn Al-Qayyim (Allaah amrehem):
“Amehabarisha Allaah kwamba kumpa fakiri kwa kificho ni bora zaidi kuliko kudhihirisha, na hebu chukua mazingatio pale alipodhibiti kuificha sadaka kwa mafakiri tu! Na wala hakusema kwa ujumla kwamba “kama mtaificha ni bora zaidi kwenu nyinyi” , hilo ni kwasababu zipo katika baadhi ya sadaka ambazo haiwezekani kufichwa kwake, kama vile kufanya maandalizi ya kuliandaa jeshi, kujenga daraja, kupitisha mto (wa maji) nk.” طريق الهجرتين
Kadhalika kutoa kwa dhahiri ili uhamasishe wengine katika kheri.
Muhusika: Ikhtiyaar ‘Ubayd
Mtarjimu: duaatsalaftz.net
Marejeo: miiraathun-Nabiyy uk.11
Imehaririwa: 11’jumaadal-uwlaa/1438H