33. Thawabu kwa atakayemnywesha mwanaadam au fakiri au akachimba kisima


1. Imepokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah (Allaah amridhie) , kwamba hakika Mtume wa Allaah (swalla Llaahu ‘alayhi wasallam) , amesema:
“Zama ambazo bwana mmoja alipokuwa akitembea , akiwa njiani akapatwa na kiu kali kabisa, mbeleni huko akapata kisima cha maji akashuka ndani yake na akanywa maji, ghafla alipokuwa akitoka akamuona mbwa ametoa ulimi wake kwa ukali wa kiu huku akiwa anakula tope.
Akasema (yule bwana):
Kwa hakika amefikwa mbwa huyu na kiu mithili ya ile iliyonipata mimi.
Kisha akashuka kisimani akakijaza kiatu chake maji na akakishikilia kwa mdomo wake mpaka alipofika juu ya kisima akamnywesha yule mbwa.
Allaah akamshukuru yule bwana na akamsamehe.
Wakauliza (Maswahaba) :
Ewe Mjumbe wa Allaah! Je , na sisi katika wanyama hawa tuna ujira!?
Akasema Mtume (swalla Llaahu ‘alayhi wasallam) :
“Katika kila kiumbe chenye ini kilicho na uhai kuna ujira (mkikifanyia ihsani muda wa kuwa ni miongoni mwa vile vifanyiwavyo ihsani)”.
Sahihi: ameipokea Bukhary (2323) , na Muslim (2244).
2. Imepokelewa kutoka kwa Sa’ad bin ‘Ubaadah (Allaah amridhie) amesema:

Nilisema kumuuliza Mtume wa Allaah (swalla Llaahu ‘alayhi wasallam) :
“Ewe Mjumbe wa Allaah! Hakika mama yangu amefariki je, naweza kumtolea sadaka!?
Akajibu (swalla Llaahu ‘alayhi wasallam):
“Naam”.
Akauliza tena:
Sadaka gani ni bora zaidi??
Akajibu (swalla Llaahu ‘alayhi wasallam):
“Ni maji”.
Akachimba kisima, kisha akasema:
“Kisima hiki ni cha mama Sa’ad (yaani: thawabu zake zimuendee yeye)”.
Hasan kwa shawaahid zake: ameipokea Abuu Daud (1681), na ibn Maajah (3684), na ibn Hbban (3337), na ibn Khuzaymah (2497), na Al-Nasaaiy (6/254).
3. Imepokelewa kutoka kwa Jaabir bin ‘Abdillaah (Allaah awaridhie) , kwamba hakika Mtume wa Allaah (swalla Llaahu ‘alayhi wasallam) amesema:
“Yeyote atakayechimba kisima cha maji, hakitoyanywa maji hayo kiumbe chochote chenye ini lililo hai, awe ni jini, mtu, au ndege , ila atalipwa na Allaah siku ya kiyama”.
Sahihi: ameipokea ibn Khuzaymah (2/269), na ameifanyia takhriij Al-Albaaniy katika “sahiih al-targhiib” (963).
Muhusika: Ikhtiyaar ‘Ubayd
Mtarjimu: duaatsalaftz.net
Marejeo: miiraathun-Nabiyy uk.11
Imehaririwa: 11’jumaadal-uwlaa/1438H