49. Thawabu za atakayefanya ‘umrah mwezi wa ramadhani


Imepokelewa kutoka kwa ibn ‘Abbas (Allaa awaridhie) , amesema:
Hakika Nabiy (swall Llaahu ‘alayhi wasallam) amesema:
” ‘Umrah katika mwezi wa ramadhani hulingana (kithawabu) na hajji, au hija pamoja nami”.
Ameipokea Bukhary na Muslim, na Abuu Daud na ibn Khuzaymah kwa urefu zaidi.
Na lafudhi iliyokuja kwa Abuu Daud amesema:
Alitaka Mtume wa Allaah (swalla Llaahu ‘alayhi wasallam) kwenda hija, akasema mwanamke mmoja kumwambia mumewe:
Niwezeshe niende hija pamoja na Mtume wa Allaah (swalla Llaahu ‘alayhi wasallam).
Akasema:
Sina cha kukubebea.
Akasema (mwanamke):
Niwezeshe kuhiji kwa yule ngamia wako fulani.
Akajibu (mume):
Yule nimemtoa wakfu katika njia ya Allaah -‘azza wajalla-.
Kisha akamwendea Mtume wa Allaah (swalla Llaahu ‘alayhi wasallam) akasema:
Hakika mke wangu anakusalimu na kukutakia rahma za Allaah. Na hakika ameniomba nimruhusu aende hija pamoja nawe, nikamwambia sina cha kukuwezeshea (kwenda hajj), akaniambia nimpe ngamia wangu fulani, nikamwambia huyo nimemtoa katika njia ya Allaah.
Akasema Mtume (swalla Llaahu ‘alayhi wasallam):
“Hakika wewe hata ungemhijisha juu yake bado angeendelea kuhesabika (ngamia huyo) yupo katika njia ya Allaah”.
Akasema tena (yule mume):
Na hakika yeye (mke wangu) amenituma nikuulize, hivi (mtu) kuhiji pamoja na wewe malipo yake ni sawa na kitu gani!?
Akasema Mtume wa Allaah (swalla Llaahu ‘alayhi wasallam):
“Mpe salamu, na umwambie kwamba sawa sawa yake ni sawa na kuhiji pamoja nami”.
Yaani kufanya ‘Umrah katika ramadhani”.
Sahihi: ameipokea Bukhary (1782), na Muslim (1256).
2. Imepokelewa kutoka kwa Abuu Twaliiq (Allaah amridhie), kwamba hakika yeye alimuuliza Nabiyy (swalla Llaahu ‘alayhi wasallam):
Hija pamoja nawe ni sawa na kitu gani!?
Akasema:
” ‘Umrah ndani ya ramadhani”.
Sahihi: ameipokea Al-Bazzar (1151), na akasema Al-Haythamiy katika “al-maj’ma’i” (3/280): (wapokezi wa Bazzar ni wapokezi wa sahiih) (3685), na hadithi ameifanyia takhriij Al-Albaaniy katika “al-sahiihah” (3096).
udadavuzi
Jumla ya kauli juu ya hizo hadithi tajwa hapo juu hubainisha malipo na fadhila za kwenda ‘umrah ndani ya mwezi wa ramadhani kwamba malipo yake ni sawa na kuhiji pamoja na Mtume (swalla Llaahu ‘alayhi wasallam).
Muhusika: Ikhtiyaar ‘Ubayd
Mtarjimu: duaatsalaftz.net
Marejeo: miiraathun-Nabiyy uk.15-16
Imehaririwa: 22’jumaadal-uwlaa/1438H