96. Thawabu katika kuomba maghfirah


 

 

◆ ثواب الإستغفار◆

عن أبي ذر رضي الله عنه ، عن النبي صلى الله عليه وسلم فيما يرويه عن الله تبارك وتعالى أنه قال: ((يا عبادي! إني حرمت الظلم على نفسي وجعلته بينكم محرما فلا تظالموا ، يا عبادي! كلكم ضال إلا من هديته فاستهدوني أهدكم ، يا عبادي! كلكم جائع إلا من أطعمته فاستطعموني أطعمكم ، يا عبادي ! كلكم عار إلا من كسوته فاستكسوني أكسكم ، يا عبادي! إنكم تخطؤون بالليل والنهار وأنا أغفر الذنوب جميعا فاستغفروني أغفر لكم)). وتقدم في ثواب الدعاء ، ورواه ابن ماجة ولفظه: قال رسول الله صلى الله عليه وسلم: ((إن الله تبارك وتعالى يقول: يا عبادي! كلكم مذنب إلا من عافيت فسولني المغفرة فأغفر لكم ، ومن علم منكم أني ذو قدرة على المغفرة فاستغفرني بقدرتي غفرت له)). فذكر الحديث

[صحيح: رواه مسلم]
Imepokelewa kutoka Kwa Abuu Dharr (Allaah amridhie) , kutoka kwa Mtume (swalla Llaahu ‘alayhi wasallam) , katika yale anayoyapokea kutoka kwa Mola wake (Allaah Tabaaraka wata’aala) , kwamba hakika yeye amesema:
→ “Enyi waja wangu! Hakika Mimi nimeiharamisha dhulma juu ya nafsi yangu , na nikaijalia baina yenu kuwa ni haramu , hivyo msidhulumiane.
→ Enyi waja wangu! Nyote nyinyi mmepotea (mmeghafilika na sharia) isipokuwa yule niliyemuongoza , hivyo niombeni mimi Uongofu nitakuongozeni.
→ Enyi waja wangu! Nyinyi nyote mna njaa , ila yule niliyempa mimi , hivyo niombeni riziki (chakula) nitakulisheni
→ Enyi waja wangu! Nyote nyinyi mpo uchi , ila yule niliyemvisha , basi Ombeni mavazi kutoka kwangu nitakuvisheni.
→ Enyi waja wangu! Hakika nyinyi mnakosea usiku na mchana , na Mimi ndiye ninayesamehe madhambi yote , basi niombeni msamaha nitakusameheni.”
Na imetangulia katika mlango wa thawabu za dua.
Na Ameipokea Ibn Maajah. Na lafudhi yake imekuja hivi:
” Amesema Mtume wa Allaah (swalla Llaahu ‘alayhi wasallam):
“Hakika Allaah (tabaarak wata’aala) anasema:
Enyi waja wangu! Nyote nyinyi ni wakosaji ila Yule niliyemuafu (kwa janga hilo) , basi niombeni msamaha nitakusameheni.
Na yeyote atakayejua miongoni mwenu kuwa Mimi ni mwenye uwezo wa msamaha , kisha akaniomba msamaha kwa kupitia (Sita ya ) uwezo wangu , basi nitamsamehe huyo”.
Sahihi: Ameipokea Muslim.

عن أبي هريرة رضي الله عنه قال: قال رسول الله صلى الله عليه وسلم: ((والذي نفسي بيده! لو لم تذنبوا ، لذهب الله بكم ، ولجاء بقوم يذنبون ، فيستغفرون الله ، فيغفر لهم))

[صحيح: رواه مسلم]
Imepokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah (Allaah amridhie) , amesema:
Amesema Mtume wa Allaah (swalla Llaahu ‘alayhi wasallam):
“Naapa kwa yule ambaye nafsi yangu ipo mikononi mwake, lau nyinyi msingelikuwa mnamkosea (Allaah) , basi Allaah angekuondoeni kisha akawaleta watu wengine ambao watafanya makosa na wamuombe msamaha Allaah , kisha akawasamehe”.
Sahihi: Ameipokea Muslim.

■ Tanbiih:■

Katika hii hadithi ya pili kuna uzindushi tunapenda kuutoa, isifahamike kimakosa hii hadithi kuwa eti miongoni mwa maana zake ni kuwa Allaah anapenda waja wake wajikurubishe kwake kwa madhambi na maasi (haashaa wakallaa!).
Kwani yeye ndiye aliyesema katika aya mbili zenye namba saba (7) ,katika ” suuratuz-zumar” na “suuratul-hujuraat):

((إِن تَكْفُرُوا فَإِنَّ اللَّهَ غَنِيٌّ عَنكُمْ ۖ وَلَا يَرْضَىٰ لِعِبَادِهِ الْكُفْرَ ۖ وَإِن تَشْكُرُوا يَرْضَهُ لَكُمْ))

“Kama mtakufuru basi eleweni kuwa Allaah ni mkwasi juu yenu (wala hana shida na utiifu wenu) , na wala haridhii kwa waja wake kufanya ya ukafiri. Na kama mtashukuru hilo analiridhia kwenu”.

Na amesema tena Allaah (Subhaanah!):

((وَلَٰكِنَّ اللَّهَ حَبَّبَ إِلَيْكُمُ الْإِيمَانَ وَزَيَّنَهُ فِي قُلُوبِكُمْ وَكَرَّهَ إِلَيْكُمُ الْكُفْرَ وَالْفُسُوقَ وَالْعِصْيَانَ ۚ))

“Lakini Allaah! Amekupendezesheeni Iymaan, na akaipamba katika nyoyo zenu , na akakuchukizeni ukafiri na ufasiki na maasi”.
Bali kubwa lililopo katika hii hadithi ni kubainisha upana wa Rehema za Allaah na msamaha wake kwa waja wake.
Na bila shaka Muislam mkosefu ambaye ni mwana wa Adamu mwenye makosa, anapotenda dhambi kisha akajua kuwa Msamaha na Rehema za mola wake zimetangulia ghadhabu zake atatubia na kurudi kwa mola wake.
Pamoja ya kuwa haijuzu kutegemea hadithi hii na kufanya ujasiri katika kutenda dhambi. Kwa sababu hatojua kuwa baada ya dhambi atakalolitenda ataendelea kuishi au laa!
Kwa sababu wapo miongoni mwa watu wanaochukuliwa roho zao wakiwa katika kutenda dhambi. Au baada tu ya kumaliza kutenda dhambi. Na lau tukikadiria kuwa atatubia huenda isipokelewa toba yake.
Kwa lugha ya jumla aliyetenda dhambi asikate tamaa juu ya msamaha na Rehema za mola wake , lakini pia kujiaminisha juu ya maasi ni jambo lisilofaa.

Na amesema ‘Allaamah Ibn Baaz (Allaah amraham):

“Maana ya hadithi ni kwamba Allaah (Subhaanah!) , ameshapitisha katika Elimu yake ya tangu kuwa lazima madhambi yatokee , ili zidhihirike athari za maghfira yake na Rahma zake (subhaanah). Na lidhihirike jina lake Al-Tawwab, Al-Ghafuur na Al-‘Afuww. Kwa sababu yeye (Jalla wa ‘alaa) lau kusingelikuwa na madhambi (yatendwayo) basi jina lake la Al-‘Afuww,Al-Ghafuur na Al-Tawwab lisingelikuwa na maana.
Hivyo yeye (Subhaanah wata’aala) , ilishatangulia katika mapitisho yake na Elimu yake kwamba majini na watu watakuja kufanya makosa (madhambi) , kisha Allaah atamsamehe amtakaye katika watakaotubia , na wala haina maana kuwa hadithi hii ni ruhusa na kibali cha kutenda dhambi. Hapana! Kwani Allaah alishayakataza na kuyaharamisha”.

Muhusika: Shaykh Ikhtiyaar ‘Ubayd

Kiunganishi: http://duaatsalaftz.net/category/makala/miirathun-nabiyy/
Mtarjim: http://duaatsalaftz.net/
Marejeo: miiraathun-Nabiyy Uk.31
Imehaririwa: 17’J-Uwlaa/1439H