30. Thawabu za kutoa sadaka na fadhila zake


1. Imepokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah (Allaah amridhie), kwamba hakika Mtume wa Allaah (swalla Llaahu ‘alayhi wasallam) amesema:

“Haipunguzi chochote sadaka katika mali, na wala Allaah hatomzidishia mja wake kwa msamaha (aliowapa waja wanzake) ila atamzidishia cheo (hadhi) , na wala hatojishusha yeyote kwaajili ya Allaah ila atainuliwa na Allaah”.
Sahihi: ameipokea Muslim (1906).
2. Imepokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah (Allaah amridhie) amesema:
Amesema Mtume wa Allaah (swalla Llaahu ‘alayhi wasallam):
“Yeyote atakayetoa sadaka kwa kima cha tende (moja) iliyotokana na chumo zuri, na wala Allaah hakubali ila vilivyo vizuri.
Na hakika Allaah atakipokea sadaka hiyo kwa mkono wake wa kuumeni kisha atailea kumlelea mwenye sadaka hiyo kama ambavyo mmoja wenu anavyomlea ndama wake, hata ile tonge (anayolisha mmoja wenu anailea na kuikuza) inakuwa kubwa mithili ya mlima uhudi”.
Sahihi: ameipokea Bukhary (1410), na Muslim (1014), na Al-Nasaaiy (5/75), na Al-Tirmidhiy (661), na ibn Khuzaymah (2425).
Na usadikisho wa hilo kwenye kitabu cha Allaah aliyetukuka:
(ألم يعلموا أن الله هو يقبل التوبة عن عباده ويأخذ الصدقات وأن الله هو التواب الرحيم (التوبة ١٠٤
“Hivi hawajui ya kwamba Allaah ndiye anayewakubaliwa waja wake toba na kupokea sadaka!? Na kwamba Allaah ni Mwingi wa kupokea toba Mwingi wa huruma”.
قال الله تعالى : يمحق الله الربى ويربي الصدقات والله لا يحب كل كفار أثيم (البقرة: ٢٧٦)
“Allaah huiondoshea baraka mali ya riba na huikuza mali yenye kutolewa sadaka, na Allaah hampendi kila mpingaji wa shari’ah mwingi wa madhambi”.
Muhusika: Ikhtiyaar ‘Ubayd
Mtarjimu: duaatsalaftz.net
Marejeo: miiraathun-Nabiyy uk.10
Imehaririwa: 11’jumaadal-uwlaa/1438H