34. Thawabu za kutoa katika njia za kheri kwa kumwamini Allaah na kumtegemea


1. Imepokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah (Allaah amridhie) , kwamba hakika Mtume wa Allaah (swalla Llaahu ‘alayhi wasallam) amesema:
“Amesema Allaah -‘azza wajalla-:
“Toa (ewe mwanaadam) nami nitakupa”.
2. Na alisema (swalla Llaahu ‘alayhi wasallam):
“Mikono ya Allaah imejaa, haipunguzwi na chochote katika utoaji wake, humimina kwa wingi (neema zake) katika nyakati za usiku na mchana.
Hamjaona ni mangapi ametoa tangu alivyoumba mbingu na ardhi!
Basi hakika hakijapungua chochote katika alivyonavyo mikononi mwake.
Na ‘Arshi yake ipo juu ya maji, na mkononi mwake kuna mizani huwashusha (watu kwayo) na kuwainua”.
Sahihi: ameipokea Bukhary (4684), na Muslim (993).
3. Na imepokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah (Allaah amridhie) , amesema:
Amesema Mjumbe wa Allaah (swalla Llaahu ‘alayhi wasallam):
“Mfano wa mtu bakhili na mwenye kutoa, ni mfano wa watu wawili waliovaa ngao ya chuma (vazi la kujikinga na silaha vitani), lililowanasa kuanzia vifuani mwao mpaka kwenye makoo yao. Ama yule mtoaji , hatotoa chochote ila ngao yake itatanuka mwili mwake mpaka kufikia kufunika vidole vyake (vya miguu), na hufuta madhambi yake.
Na ama yule mtu bakhili ambaye hana tabia ya utoaji , ile ngao itambana na atajaribu kuitanua lakini haitotanuka”.
Sahihi: ameipokea Bukhary (5797), na Muslim (1021).
Uchambuzi
Katika hadithi ya mwisho , Mtume (swalla Llaahu ‘alayhi wasallam) , amejaalia mfano wa mtu mtoaji kuwa ni sawa na mtu aliyevaa ngao iliyomsitiri mwili mzima.
Na amejaalia mfano wa mtu bakhili kuwa ni sawa na mtu ambaye ameifunga mikono yake hivyo ngao ikashindwa kumsitiri mwili mzima ikabaki inamkaba sehemu ya kifua na koo.
Makusudio ya mfano huu ni kuwa , mtu mkarimu na mtoaji anapodhamiria kutoa basi moyo wake huwa mwepesi na unatanuka (kama ilivyotanuka ngao kwenye mwili), halikadhalika mikono yake inamtii na kukunjuka kwa utoaji (kama ilivyomtii kwenye ngao ambayo ilivuka mikono miwili ambayo haikufungwa kwa utoaji, na kusababisha ngao kushuka mpaka chini ya miguu yake). Na hapo ndipo anapositiriwa na Allaah mtoaji kwa aibu zake na kusamehewa kwa madhambi yake.
Muhusika: Ikhtiyaar ‘Ubayd
Mtarjimu: duaatsalaftz.net
Marejeo: miiraathun-Nabiyy uk.12
Imehaririwa: 14’jumaadal-uwlaa/1438H