19. kutorikodi sauti wala maandishi ya Mtoa fat’wa bila ya idhini yake


Miongoni mwa adabu zichungwazo kwa muulizaji ni kwamba anapowauliza Wanazuoni kwa njia ya simu au isiyokuwa ya simu asirikodi jawabu kimaandishi wala kwa kinasa sauti ila kwa idhini ya Mwanazuoni.
Na ilishanitokea kuona baadhi ya ndugu kurikodi jawabu la mmoja wa Wanazuoni jambo ambalo halikupasa. Na haya yote ni kwasababu ‘Aalim anajibu kwa kadri ya jinsi alivyoulizwa, na lau angejua kwamba muulizaji anamrikodi na kwamba jawabu litasikiwa na watu wengine pia bila shaka jawabu lake lingebadilika lisingekuwa kama la kwanza.
Hivyo, miongoni mwa utovu wa nidhamu na kutochunga haki zao na kujali ni kurikodiwa kwa majibu ya Wanazuoni kwa njia ya simu au uandishi kisha yakatawanywa bila ya idhni zao. Kwasababu wao ndio wenye haki ya kuidhinisha kusambazwa kwa fatawa zao au laa.
Na muulizaji alipouliza aliuliza yanayomuhusu yeye kama yeye, je, ‘Aalim alikupa idhini pale ulipomuuliza urikodi swali na jawabu lake kwa njia ya simu!? Jawabu ni kwamba hajakuidhinisha. Sasa ukitaka kumrikodi ulipaswa umuombe idhini kabla , na umwambie:
Allaah akupe mazuri ewe Sheikh! Nilikuwa naomba kurikodi jawabu kwenye kanda naomba uniruhusu basi nirikodi!
Kama atakuidhinisha hapo utakuwa umetekeleza adabu ipasavyo, na wala hutohesabika katika wale wasio na adabu kwa Wanazuoni wanaotumia vibaya fursa wakawarikodi kwa wasiyopenda kurikodiwa.
Muhusika: Shaykh Swaalih Aalish-Shaykh
Mtarjimu: duaatsalaftz.net
Marejeo: adabus-suaal uk.25
Imehaririwa: 28’jumaadal-uwlaa/1438H