09.Faida Katika Hadeeth ya Jibriyl-04


(2). Inapendekezwa kwa Mahujaji na wanaofanya ‘Umrah kwa mnasaba wa kwenda kwao katika miji Mitukufu wajifunze Dini na kuwaejea Wanazuoni katika kutaka kujua mambo yanayowatatiza miongoni mwa hukumu za Dini (ya Kiislam). Kama ilivyotokea kwa Yahya bin Ya’mar na Humayd bin ‘Abdir-Rahman Al-Himyariy katika kisa hiki.
Na miongoni mwa natija nzuri ambazo atazipata yule aliyeafikishwa na Allah ni kujifunza Dini na kusalimika kutokana na kutumbukia katika shari. Kama ilivyokuja hadithi katika “Sahihi Muslim” (191) kutoka kwa Yaziidil-Faqiir amesema:
Nilikuwa nimependezwa na mtazamo miongoni mwa mitazamo ya Khawārij, tukatoka katika kikosi cha watu wengi tukikusudia kuhiji, kisha tujetuwafanyie watu uasi. (Anasema): Tukapita Madinah mara tukamkuta Jābir bin ‘Abdillāh akiwahadithia watu kutoka kwa Mtume (swalla Llāhu ‘alayhi wasallam) huku akiwa ameegemea nguzo. (Anasema): Mara akawataja watu wa motoni. Nikamwambia: Ewe Swaha wa Mtume wa Allāh! Ni mambo gani haya mnayosimulia? Ilhali Allāh anasema:

“إِنَّكَ مَن تُدْخِلِ النَّارَ فَقَدْ أَخْزَيْتَهُ ۖ      ” آل عمران١٩٢

“Hakika utakayemuingiza motoni basi huyo umemfedhesha” Al-‘Imrān (192).
Na amesema:

“كُلَّمَا أَرَادُوا أَن يَخْرُجُوا مِنْهَا أُعِيدُوا فِيهَا      ” السجدة ٢٠

“Kila wanapotaka kutoka (kwenye Jahannam) hurudishwa humo” Al-Sajdah (20)._
Akasema Jābir: Je, unasoma Qur’an?
Nikasema: Ndiyo.
Akasema: Je ulishasikia kuna “Maqaam” ya Muhammad (‘alayhis-salaam) atakayowekwa?
Nikasema: Ndiyo.
Akasema: Hakika hiyo ni Maqaam ya Muhammad (swalla Llāhu ‘alayhi wasallam) atakayehimidiwa ambaye Allāh atawatoa (kutoka motoni) kupitia yeye awatakao.
Kisha akaizungumzia Syraat na jinsi watu watakavyoipita.
Anasema: Naogopa huenda nisiwe nimeyahifadhi hayo, ila alisema kuwa kuna watu watatoka motoni baada ya kuwa humo. Watatoka wakiwa kama miti ya simsim, kisha wataingia kwenye mto miongoni mwa mito ya pepo kisha wataogelea humo na kutoka wakiwa kama vile karatasi. Kisha tukarudi huku tukisema: mna nini nyinyi!? Mnadhani kuwa Shaykh atamsingizia Mtume (swalla Llāhu ‘alayhi wasallam)? Kisha tukarudi zetu na wallah hakuna aliyetoka miongoni mwetu ila bwana mmoja tu, au kama alivyosema Abū Nu’aym” .
ambaye ni Al-Fadhl ibn Dukayn ambaye ni mmoja wa watu wa Isnadi.
Kikosi hiki kilikuja hajj na walikuwa wametahiniwa kwa ufahamu wa kimakosa, nao ni kuwa waliofanya madhambi makubwa hawatotoka motoni. Na wakazibeba zile ayah zinazowahusu makafiri juu ya Waislam pia, na bila shaka hili ni miongoni mwa itikadi za Khawārij. Na walikusudia baada ya kurudi hajj waje kupambana na watu kwa itikadi yao hii batili. Lakini kwa hii safari nzuri (ya Hajj) Allāh aliwapa tawfiiq ya kukutana na Jābir bin ‘Abdillāh Al-Answāriy (Allāh awaridhie) akawabainishia ubaya wa uelewa wao wakaachana na lile (baya) walilokuwa wameliazimia. Na hakuna aliyetoka kwa batili waliyoiazimia miongoni mwao ila mtu mmoja tu.

 

 

Muhusika: Shaykh ‘Abdul-Muhsin Al-‘Abbād Al-Badr
Mtarjim: http://duaatsalaftz.net/
Marejeo: Sharh Hadithi Jibriil