25.Faida Katika Hadithi Ya Jibriil- 20


Yapili (ب):

Na shahada ya لا إله إلا الله maana yake ni: Hakuna wa kuabudiwa kwa haki isipokuwa Allāh. Na neno hili ambalo ni la Ikhlās limebeba nguzo kuu mbili:

1) Kukataa mwanzoni mwake.
2) Kuthibitisha kilicho mahsusi mwishoni mwake.

Mwanzoni mwake linakataa ibada kwa asiyekuwa Allāh.

Na mwishoni mwake linathibitisha Ibada kwa Allāh pekee asiye na mshirika.

Na khabar ya “لا” ambayo inakana jinsi ya vitu, makadirio yake huwa ni “حق”, na wala haitokuwa sawa ikadiriwe “موجود”, kwa sababu waungu wa batili wapo tele,[1] lakini kinachokanwa ni Uungu wa haki, kwani huo haupo kwa asiyekuwa Allāh, na unathibitishwa kwa Allāh pekee.

————————-
[1] Tafsiri ya neno kwa neno ilikuwa iwe “Hakuna Mola (Muabudiwa) isipokuwa Allāh”, lakini kilugha hiyo herufi لا, ambayo inakataa jinsi ya vyote vinavyoabudiwa inahitajia kuwekea khabar yake (kwa mujibu wa lugha ya kiarabu), sawa wapo wanaokosea wakakadiria khabari yake ni kusema “موجود” , kwa maana “aliyepo”, hivyo kwa mujibu wa makadirio hayo itakuwa maana ya hilo kalimah “Hakuna Muabudiwa aliyepo isipokuwa Allāh”, na bila shaka kukadiria kwa makadirio haya ni kosa linalopingana na uhalisia, kwani uhalisia unasema waabudiwa wapo wengi.

-Tupu zinaabudiwa barahindi
-Ng’ombe wanaabudiwa barahindi.
-Mapango yanaabudiwa hata hapa kwetu.
-Misitu na makaburi yanaabudiwa.
-Mizimu inaabudiwa
-Malaika wanaabudiwa.
-Jua na Mwezi vinaabudiwa.
-Manabii na waja wema wanaabudiwa.

Kwa hiyo haitofaa kuikadiria (kilugha) khabar ya لا, iliyopo katika kalimah ya Tawhiid kwa kusema “موجود”, kwakuwa vinavyoabudiwa kinyume na Mola Qahhār vipo vingi, bali sawa sawa yake ni kukadiriwa khabar ya herefi لا, kuwa ni “حق”, ambayo itabeba maana ya sawa na kusema: “Hakuna Muabudiwa wa haki isipokuwa Allāh”, na ukikadiria hivyo utakuwa umeusibu usawa na kupatia.

 
 
 
Muhusika: Shaykh’Abdul-Muhsin Al-‘Abbād Al-Badr
Mtarjim: http://duaatsalaftz.net/
Marejeo: Sharh Hadith Jibriil