38.Faida Katika Hadithi Ya Jibriil – 33


Yatatu (د):

Amepokea Muslim katika Sahihi yake (654), kutoka kwa Ibn Mas’uud (Allāh amridhie), kuwa amesema:
“Yeyote atakayependezwa na kukutana na Allāh kesho (kiyama) akiwa ni Muislam wa sawa sawa, basi na azichunge hizi swala (tano) pale unapolingana mlingano wake (adhana), kwani hakika Allāh amemuekea Nabii Wenu (swalla Llāhu’alayhi wasallam) njia za Uongofu, na hizo (swala) ni miongoni mwa njia za Uongofu. Na lau kama nyinyi mtakuwa mkiswali majumbani mwenu kama anavyoswali huyu mzembeaji katika nyumba yake, mtakuwa mmeuacha mwenendo wa Nabii wenu. Na mtakapouacha mwenendo wa Nabii wenu bila shaka mtapotea[1]. Na hakuna mtu yeyote ambaye atajitwaharisha vyema (nyumbani kwake), kisha akatoka na kuelekea katika Msikiti miongoni mwa Misikiti hii, isipokuwa Allāh atamwandikia kwa kila hatua atakayoiinua Jema moja, na atamrufaisha kwayo daraja, na atamfutia kwayo baya moja. Na hakika tulijikuta sisi tukionelea ya kuwa hakuna atakayeizembea swala (kwa Jamaa) isipokuwa ni yule mtu mnafiki mwenye kujulikana kwa unafiki wake Na alikuwa mtu (mgonjwa) analetwa (kwenye swala) akiwa anachechemea huku akiwa anawaegemea watu wawili mpaka wamfikishe katika safu”.
———————-
[1] Na katika mapokezi mengine ya Abū Daud alisema “Mtakufuru” badala ya mtapotea.
 
 
 
Muhusika: Shaykh’ Abdul-Muhsin Al-‘Abbād Al-Badr
Mtarjim: http://duaatsalaftz.net/
Marejeo: Sharh Hadith Jibriil