44.Faida Katika Hadithi Ya Jibriil – 39


Yasita:

Kuhiji katika nyumba ya Allāh Tukufu ni Ibada ya kimali na kiwiliwili. Allāh ameiwajibisha kwa umri wa mtu mara moja. Na amebainisha Mtume (swalla Llāhu’alayhi wasallam) fadhila zake kwa kauli yake aliposema:

من حج فلم يرفث ولم يفسق رجع كيوم ولدته أمه”

“Atakaehiji kisha asiseme machafu wala asifanye mabaya atarudi kama siku aliyozaliwa na mama yake”.
Ameipokea Bukhari (1820), na Muslim (1350).
Na kauli yake (swalla Llāhu’alayhi wasallam):

“العمرة إلى العمرة كفارة لما بينهما، والحج المبرور ليس له جزاء إلا الجنة”

“Umrah mpaka Umrah ni kifutio cha madhambi yaliyotendwa baina yake, na Hija iliyotakaswa haina malipo zaidi ya Pepo”.
Ameipokea Muslim (1349).
Na uwezo wa kuiendea Hija unakuwa ni wa kiwiliwili na mali pamoja
Na inafaa kumhijia maiti.
Ama aliyehai haitofaa kuhijiwa ila katika hali mbili:
1) Awe ni mzee kikongwe ambaye hawezi kusafiri.
2) Awe ni mgonjwa mwenye maradhi yasiyotarajiwa kupona.
Na katika uwezo kwa mwanamke ni kuwa na Mahram wake, pale atakapokuwa ametokea nje ya mji wa Makkah. Kwa ushahidi wa maneno yake Mtume (swalla Llāhu’alayhi wasallam):
“Asipwekeke mtu na mwanamke ila awe na Mahram wake, na wala asisafiri mwanamke ila awe na Mahram wake. Akasema bwana mmoja: Ewe Mtume wa Allāh! Hakika mke wangu ametoka kwenda Hija, na mimi nipo kwenye orodha ya watakaoshiriki vita fulani na vita fulani. Akasema Mtume (swalla Llāhu’alayhi wasallam): Nenda kahiji na mkeo”.[1]
Ameipokea Bukhari (3006), na Muslim (1341), kutoka katika Hadithi ya Ibn Abbas (Allāh awaridhie).
——————–
[1] Katika makosa makubwa yanayofanywa na baadhi ya Taasisi za Hajj hata zile zinazojinasibu kufuata Sunnah, ni kuwachukua wanawake bila ya Mahram zao, wakati Shari’ah imekataza jambo hilo la kusafiri kwa mwanamke hata kama ni safari ya Hajj bila ya Mahram wake.
Amesema Shaykh Al-Uthaymiin (Allāh amraham):
“Tunatakiwa tuwatulize dada zetu ambao hujiskia vibaya na kukumbwa na huzuni pale wanapokosa Mahram, na tuwaambie waondoe shaka hata kama mtakwenda kukutana na Allāh bila ya Hija basi hakutokuwa na kitu juu yenu, kwanini? Kwa sababu Hija (kwa mazingira haya) si wajibu juu yenu. Kama ambavyo fakiri atakapokutana na Mola wake ilhali hajatoa zaka, kutakuwa na lolote juu yake? Bila shaka hakuna lolote juu yake kwa sababu hana mali. Hivyo Alhamdulillaah juu ya Neema zake, yaani inatakikana tuwatulize wanawake, kwa sababu baadhi ya wanawake wanapatwa na huzuni kali, mpaka inatokea baadhi yao wanamuasi Allāh (kwa kuhiji) bila ya Mahram, SubhānaLlaah! Vipi unajikurubisha kwa Allāh kwa kumuasi? Hili ni kosa kubwa sana na upumbavu” Rej: Sharh Al-Kabāir (Uk. 72-73).
Na kamati ya kudumu ya kutoa fat-wah (Allajnatud-Dāimah), imesema haya:
“Usahihi ni kwamba haifai kwake (mwanamke) kusafiri kwaajili ya Hija isipokuwa aongozane na mumewe au Mahram wake katika wanaume, hivyo haitofaa kwake kusafiri na kundi la wanawake waaminifu ambao si Mahaarim, au kusafiri na shangazi yake au mama yake mdogo)mkubwa, au mama yake (mzazi), bali ni lazima awe na mumewe au Mahram wake katika wanaume, asipopata wakusuhubiana naye miongoni mwa hao basi hakutokuwa na wajibu wa Hija juu yake muda wa kuwa atakuwa katika mazingira hayo”.
 
 
Muhusika: Shaykh ‘Abdul-Muhsin Al-‘Abbād Al-Badr
Mtarjim: http://duaatsalaftz.net/
Marejeo: Sharh Hadith Jibriil