06.Kumwokoa Mfamaji na Kuangaza Njia


5- Ni upi msimamo wa Ahlus-Sunnah kuhusu yale yaliyojiri baina ya Swahaba (Allāh awaridhie)??
Jibu- Wanajizuilia kutokana na kuyasema yale yaliyojiri baina ya Maswahaba. Na wanasema ya kuwa: hizi habari zilizopokelewa juu ya mabaya yao, zipo ambazo ni uongo, na nyingine zimeongezwa (chumvi) na kupunguzwa, na ziko ambazo zimegeuzwa kutokana na uhalisia wake.
Na neno sahihi kuhusu wao ni kwamba; wanapewa udhuru, kwani wao ima wawe wamejitahidi wakapatia, au wamejitahidi wakakosea.
Na wao (Ahlus-Sunnah) pamoja na yote hayo, hawaitakidi kuwa kila mmoja katika Maswahaba amekingwa kutokana na makosa makubwa na madogo, bali yawezekana kupatikana kutoka kwao makosa kwa ujumla, na wao wana vitangulizi vizuri na fadhila ambazo huwajibisha kusamehewa kwa makosa ambayo yatatokea kutoka kwao.
Mpaka wanasamehewa madhambi ambayo msamaha huo huenda wasiupate waliokuja baada yao, kwa sababu wao wana mema yanayofuta mabaya ambayo hawanayo (mema) hayo waliokuja baada yao.
Na imeshathibiti kutoka kwa Mtume wa Allāh ﷺ kusema kuwa: Wao ni bora ya Karne. Na kwamba mmoja wao akitoa kibaba cha sadaka huwa ni bora zaidi kuliko dhahabu ya mlima wa uhudi kwa wale watakaokuja baada yao.
Kisha kama itatokea mmoja wao katenda dhambi, basi inayumkinika kuwa ametubia, au amefanya mema (baada ya dhambi hilo) ambayo yatalifuta (hilo dhambi), au akawa amesamehewa kupitia fadhila za utangulizi wake (katika Iymān), au kupitia maombezi ya Mtume Muhammad ﷺ , na wao wana haki zaidi ya uombezi wake kuliko wengine. Au akapewa mtihani hapa duniani ambao utakuwa ni kafara ya dhambi lake.
Na hapa ni kwa yale madhambi ambayo yamehakikika (kwao), vipi itakuwa kwa yale mambo ambayo wao walifanya jitihada? Bila shaka kama watapatia watalipwa mara mbili, na watakosea watalipwa ujira mmoja na kosa kusamehewa.
Kisha hayo makosa ambayo yametokana na wao ni machache mno, yatamezwa na bahari ya mema yao, miongoni mwa Iymāni zao kumwamini Allāh na Mtume wake, na kuipigania njia yake, na kuhama, na kunusuru, na elimu yenye manufaa, na matendo mema.
Na atakayetazama kwa makini mwenendo wa hawa watu, kwa elimu na uoni, na yale ambayo wameneemeshwa na Allāh katika mambo ya fadhila, atajua kwa yakini kabisa kwamba wao ni bora ya viumbe baada ya Manabii, hakuna wala hawatopatikana mfano wao.
Wao ni wateule kutoka kwenye karne zote za Ummah huu ambao ni bora ya Ummah wenye utukufu zaidi mbele ya Allāh.
 
 
 
Muhusika: Ibn Taymiyyah Al-Harrāniy
Kiunganishi: http://duaatsalaftz.net/category/makala/kumwokoa-mfamaji/
Mtarjim: http://duaatsalaftz.net/
Marejeo: Al-Wāsitwiyyah Uk. 201-202
Imehaririwa: 11 Swaffar/1441H