10.Kumwokoa Mfamaji na Kuangaza Njia


9- Ni yapi waliyoyazua wazushi katika siku ya ‘Aashūraa?
      Jibu- Baadhi ya wazushi wamezua katika siku ya ‘Aashūraa uzushi wa kushinda na kiu, huzuni, mikusanyiko na mengineyo miongoni mwa mambo yaliyozuliwa ambayo hayajawekwa katika Shari’ah na Allāh Mtukufu wala Mtume wake ﷺ, wala yeyote miongoni mwa wema waliotangulia. Si katika Ahli Bayt Rasuulillah ﷺ wala wengine wasiokuwa wao.
Lakini Allāh alipomkirimu katika siku hii (ya Āshura) mjukuu wa Mtume wake, ambaye ni mmoja wa mabwana (sayyid) wawili wa vijana wapeponi, yeye pamoja na sehemu ya familia yake, kuingia mikononi mwa watu waovu waliodhalili, na tukio hili likawa ni msiba (mkubwa) kwa Waislam, ikawa ni wajibu kuupokea msiba huu kwa yale tunayopokelea misiba mingine, kwa kusema:

إنا لله وإنا إليه راجعون

Lakini sivyo walivyofanya watu wazushi katika siku kama hii, wamefanya kinyume na alivyoamrisha Allāh wakati wa misiba, wakaongeza na mengine (mabaya) kama vile kuzua uongo, na kuwazungumza vibaya Maswahaba walio mbali na hatia ya fitnah ya Husein (Allāh amridhie), na fitnah nyingine, wakataja chungu ya mambo, katika yale ambayo hayapendi Allāh na Mtume wake ﷺ.
Ilhali imepokelewa kutoka kwa Fātwimah bint Al-Husein, kutoka kwa baba yake (ambaye ni) Husein bin Aliyy (Allāh awaridhie), amesema:
Amesema Mtume wa Allāh ﷺ:
“Yeyote atakayepatwa na msiba, pale atakapoukumbuka msiba wake akasema: “Hakika sisi ni wa Allāh, na hakika sisi kwake ni wenye kurejea” hata kama muda utakuwa umesonga mbele, ataandikiwa na Allāh ujira mithili ya ujira alioupata siku ile ya ule msiba”.
Ameipokea Ahmad na Ibn Mājah.
Hebu chukua hapo mazingatio, jinsi ya kulekuwa hadithi hii ameipokea Husein (Allāh amridhie), na kutoka kwake ni bint yake aliyeshuhudia maswaibu ya baba yake!!.
Ama jambo la kufanya siku kama hizi kuwa ni siku za kufanya matanga na kudhihirisha maombolezo, haya si katika Dini ya Waislamu, bali haya matendo kunasibishwa na dini ya jaalihiyyah yana ukaribu zaidi (kuliko kunasibishwa na Dini ya kiislam).
Kisha wakanyimwa kwa sababu ya mambo yao hayo (ya kizushi) fadhila za kuifunga siku hii.
Na wakazuwa pia baadhi ya watu katika siku hii mambo ambayo yanaegemezwa kwenye hadithi mbovu ambazo hazina asili, mfano:
  1. – fadhila za kuoga katika siku hii.
  2. – kupaka wanja.
  3. – kupeana mikono.
Na mambo haya na mfano wake ni mambo ya kizushi yanayochukiza. Na jambo ambalo limesuniwa ni kufunga tu (hakuna jenginelo).
Na pia kuna riwaya zinazoruhusu watu kujipa wasaa (wa kula na kunywa pamoja na kuvaa vizuri) katika familia zao.
Na kubwa za hizo riwaya ni hadithi ya Ibrahim bin Muhammad bin Al-Muntashir, aliyepokea kutoka kwa baba yake kwamba amesema:
“Tumefikiwa na habari ya kwamba yeyote atakayewapa wasaa watu wa nyumbani kwake siku ya ‘Aashūraa, basi na yeye atapewa wasaa na Allāh mwaka mzima”.
Lakini kinachodhihiri ni kwamba hii imetungwa kipindi kile ambacho ubaguzi ulipokuwa dhahiri baina ya Nāswibah na Rāfidhwah, kwani Kundi moja liliifanya siku ya ‘Aashūraa kuwa ni siku ya maombolezo, hivyo kundi la pili likatunga hadhithi zinazowataka watu wajiachie na kujipa wasaa (katika vyakula, vinywaji na mavazi), na kuifanya siku hiyo ni sikukuu, na yote mawili ni makosa.
 
 
Muhusika: Ibn Taymiyyah Al-Harrāniy
Kiunganishi: http://duaatsalaftz.net/category/makala/kumwokoa-mfamaji/
Mtarjim: http://duaatsalaftz.net/
Marejoe: Iqtidhaa Jz 2, S 624-627
Imehaririwa: 25 ‘Rabiul 1/1441H