48.Faida Katika Hadithi ya Jibriil – 43


Ya kwanza (ب):

  • Na kumpwekesha kwa Rubuubiyyah:
Maana yake ni kule kukiri kuwa yeye ni mmoja katika matendo yake, hana mshirika katika hayo. Kama vile kuumba, kuruzuku, kuhuyisha, kufisha, kuyaendesha mambo (yote), kuiendesha dunia, na mengineyo katika yale ambayo yanafungamana na Umola wake na ulezi.
  • Na kumpwekesha kwa Uluuhiiyyah:
Maana yake ni kumpwekesha kupitia matendo ya waja,[1] kama vile kumuomba[2], kumkhofu [3], kumtaraji [4], kumtegemea, kumuomba msaada, kumuomba kinga, kumuomba uokovu, kumchinjia, kumuekea nadhiri [5], na yasiyokuwa hayo katika aina za Ibada ambazo ni wajibu kumpwekesha yeye kwazo. Hivyo haitofaa kuielekeza aina moja ya hizo kwa asiyekuwa yeye, hata kama atakuwa ni Malaika aliyekurubishwa au Nabii aliyepewa Utume achilia mbali wasiokuwa hao.

 

———————
[1] Yaani: Waja hawatoruhusika abadan kuzielekeza hizi Ibada zote au baadhi yake isipokuwa kwa Allāh pekee, na watakapozielekeza kwa asiyekuwa Allāh watatoka katika Uislam, na watakuwa washirikina waliomkufuru Allāh, na wakifa bila ya kutubia juu ya ushirikina wao huo watakuwa ni wa milele katika moto wa Jahannam.
[2] Kuomba (Dua) ni Ibada, aombwe Allāh pekee, na kwamba atakayeyaelekeza maombi yake kwa asiyekuwa Allāh katika lile ambalo haliwezi isipokuwa Allāh bila shaka atakuwa amefanya shirki kubwa inayomtoa katika mila ya Kiislam. Kama wale wanaoomba kwenye mizimu, makaburi ya Mawalii na wanaoitwa Masharifu, wanaoomba kwenye tambiko na jadi zao, wanaomuomba Abdul-Qaadir Al-Jaylaniy, au Abul-Hasan Al-Shaadhiliy na wengineo. Na wala haitokuwa shirki kumuomba mtu kalamu, chakula na mengineyo katika yale ambayo anayeombwa anao uwezo wa kumsaidia aliyemuomba.
[3] Na khofu zipo za aina tatu:
  1.  Khofu ya kimaumbile. Kama vile mtu kumkhofu mnyama mkali, au kukhofu kuungua kwa moto, au kuzama kwenye maji nk. Aina hii halaumiwi mtu juu yake, japo haitakiwi aina kama hii ya khofu iwe ni sababu ya Mtu kuacha kufanya la wajibu au akafanya la haramu.
  2. Khofu ya Ibada. Na hii inatakiwa akhofiwe Allāh tu. Na kuielekeza khofu hii kwa asiyekuwa Allāh ni shirki.
  3. Khofu ya siri. Kama vile mtu akawa anamkhofu aliyekaburini, au anamkhofu fulani Walii ambaye yupo mbali naye, ambaye hana uwezo wa kumuathiri kwa chochote lakini bado akawa anamkhofia, hii pia nayo inaingia katika khofu ya shirki.
[4] Matarajio yenye udhalili na unyenyekevu ndani yake ni Ibada inayopasa kuelekezwa kwa Allāh pekee, na kuielekeza kwa asiyekuwa Allāh ni shirki. Mfano wa matarajio ambayo ni shirki ni mtu kutaraji kupitia talasimu ambalo amelitundika dukani kwake kuwa litamletea wateja au kumkinga na madhara ya kibiashara na maafa yake. Na matarajio ambayo ni Ibada hayawi ila kwa anayefanya twa’ah kwa Allāh kisha akataraji kutoka kwa Allāh thawabu za utiifu wake. Au akawa ametubia kwa Allāh kutokana na maasi yake akataraji kukubaliwa kwa toba yake. Ama kutaraji kutoka kwa Allāh bila ya kutenda ni kujidanganya.
[5] Wapo wanaoweka nadhiri (ahadi) kwa mashetani na waganga wa kienyeji kuwa mambo yao kama yatafanikiwa baada ya kufanyiwa wanazoziita tiba, basi ima watachinja mnyama mwenye miguu minne, au watatoa sadaka Msikitini au wataleta chano mzimuni, au watagawa peremende kwa watoto wa mitaani. Na aina hii ya Nadhiri ni shirki inayomtoa mtu katika mila ya Kiislam. Nadhiri ni Ibada inayopasa ielekezwe kwa Allāh peke yake.

 

 

Muhusika: Shaykh ‘Abdul-Muhsin Al-‘Abbād Al-Badr
Mtarjim: http://duaatsalaftz.net/
Marejeo: Sharh Hadith Jibriil