49.Faida Katika Hadithi ya Jibriil – 44


Ya kwanza (ت):

  • Kumpwekesha katika Majina na Sifa.
Ni kumthibitishia katika Majina na Sifa yale aliyojithibitishia yeye mwenyewe au aliyothibitishiwa na Mtume wake (swalla Llāhu’alayhi wasallam), kwa namna ambayo inalingana na Ukamilifu na Utukufu wake. Pasi na kuziulizia zikoje, au kuzimithilisha, pasi na kuzikengeusha maana au kuzipinga na kuzikataa. Na kumtakasa na kumkania kwa kila ambalo halilingani na yeye. Kama alivyosema Allāh ‘Azza wajalla-:
لَيْسَ كَمِثْلِهِ شَيْءٌ ۖ وَهُوَ السَّمِيعُ الْبَصِيرُ (11)
“Hakuna chochote chenye mfano wake na Yeye ni Mwingi wa Usikivu na Muoni”.
Al-Shūra (11).
Akajumuisha katika Ayah hii baina ya kuthibitisha na kukanusha.
Kuthibitisha ni pale aliposema:
“Na Yeye ni Mwingi wa kusikia na kuona”.
Na kukana pale aliposema:
“Hakuna chochote chenye mfano wake”.
Hivyo anao yeye (Subhānah) Usikivu, lakini si sawa na usikivu wa wengine [1]. Na anaona lakini si sawa na kuona kwa wengine [2], Na hivi hivi ndiyo tutakavyosema kwa kila litakalothibiti kwa Allāh (Mola wetu) iwe ni katika majina au sifa.
——————-
[1] Usikivu wake umekamilika hauna dosari wala aibu na mapungufu. Tofauti na usikivu wa viumbe wake. Yeye katika kusikia kwake hachanganyikiwi kwa lugha na sauti za waombaji na wingi wao. Anasema Aisha (Allāh amridhie):
“Sifa zote njema anastahiki yule ambaye Usikifu wake umezienea sauti zote. Hakika alikuja Mujaadilah akimshitakia Mtume (swalla Llāhu’alayhi wasallam), na mimi nikiwa katika upande wa hiyo hiyo nyumba lakini sikuwa nikisika anayoyasema. Kisha Allāh akateremsha kauli yake:

قَدْ سَمِعَ اللَّهُ قَوْلَ الَّتِي تُجَادِلُكَ فِي زَوْجِهَا  ” المجادلة (١)

“Hakika amesikia Allāh kauli ya mwanamke ambaye anakuhoji kuhusu mume wake”.
Al-Mujaadilah (1).
Ameipokea Al-Bayhaqiy katika “Al-Asmaa Wassifāt”.
[2] Anamuona mdudu chungu mweusi aliyepo ndani ya pango jeusi katika giza nene la usiku. Bali anayaona yapitayo katika nafsi na dhamira zetu.
Na katika maana ya kumpwekesha kwa majina yake ni kutomwita yeyote kwa jina lake, wala kutohowa kutoka katika jina la Allāh jina la mwabudiwa mwengine, kama walivyofanya Maquraysh wakatohoa kutoka kwenye jina lake “Al-Mannān” jina la mungu wao “Manaata”, na kwenye jina la “Allāh” wakatohoa jina “Allaata”, na kwenye jina “Al-Aziiz” jina la mungu wao “Uzzaa”. Pia haifai kumwita Allāh kwa jina ambalo hajajiita yeye mwenyewe katika Qur’an, wala hajaitwa kwa jina hilo na Mtume wake Muhammad (swalla Llāhu’alayhi wasallam) katika Sunnah.

 

Muhusika: Shaykh ‘Abdul-Muhsin Al-‘Abbād Al-Badr
Mtarjim: http://duaatsalaftz.net/
Marejeo: Sharh Hadith Jibriil