Hukmu Ya Kupiga Mswaki Mchana Wa Ramadhan


Swali:

swali langu ni kwamba nini hukumu ya kupiga mswaki mchana wa ramadhani/swaumu..kusukutua mdomoni..kupandisha maji puani..kuingiza kitu mdomon isipokuwa nyenye utamu…na kujisugua mdomoni naombeni msaada wa maswali hayo majibu ningependekeza nitumiwe kwa njia ya email hapo juu kama itakua bora Zaidi

Jawabu:

الحمد لله رب العالمين، والصلاة والسلام على رسول الله محمد بن عبد الله وآله وصحبه.

Ama kuhusu suala la kupiga mswaki mchana wa Ramadhani hilo halina katazo tulijualo Kishari’ah.

Bali inafaa kupiga mswaki siku zote.  Na baadhi ya wakati huwa jambo hilo ni Sunnah inayokokotezwa.  Kama vile kinywa kinapobadilika harufu , anapoamaka mtu kutoka usingizini nk.

Ila anayepiga mswaki  akiwa ana funga iwe ya Ramadhani au nyenginezo anatakiwa kuchunga maji maji ya mti anaoswakia (mti mbichi) asiyameze wala vinyuzi vya mswaki wake huo.

Na ikitokea amevimeza hivyo kwa kudhamiria  hali ya swaumu yake  itakuwa kama anavyosema Al-Imaam Al-Nawawiy (ALLAAH Amraham!):

يفطر بلا خلاف، صرح به الفوراني ،وغيره. انتهى

“Atakuwa amefungua bila ya khilafu (katika hilo). Ameyazungumza hayo kwa uwazi Al-Fawraaniy na wengineo”.   Rej “al-maj’muu 6/318”.

Sambamba na hilo ni kupiga mswaki wenye dawa ya meno.

Hawajakataza Wanazuoni wetu jambo hilo muda wa kuwa mpiga mswaki huyo akiwa atachunga mate yenye utamu wa dawa yasitumbukie tumboni mwake.  Na hili amelifutu Al-‘Allaamah Ibn Baaz , Ibn ‘Uthaymiin (ALLAAH Awarham!), pia ni fat’wa ya Al-Imaam Al-Fawzaan (ALLAAH Amhifadhi!).

Japo Ibn ‘Uthaymiin (ALLAAH Amraham!), anaonelea kuacha kutumia dawa ni bora zaidi kuliko kuitumia kwake.

Rej “fataawa ramadhaan 2/494- 497”.

Ama kuhusu kusukutuwa:

Ikiwa inawezekana mchana wa Ramadhani kupiga mswaki basi kusukutua ni jambo lenye kufata nyuma yake .

Hivyo hakuna ubaya kusukutua japo baada ya usukutuaji huo maji hatakiwi kuyameza bali atayatema.

Bali jambo la kusukutua lipo kwenye kushika udhu pia.

Na hakuna atakayesema kuwa mwenye swaumu haruhusiwi kuchukua udhu.

Kadhalika kupandisha maji puani hilo halina makatazo wala ubaya.

Zaidi tu huruhusiwi kuyapandisha sana kwa dhana ya kuwa huenda yakakuponyoka na kuingia kooni kwa tundu hizo za pua.

Amesema Mtume (Swalla LLAAHU ‘alayhi wasallam) , kumwambia Laqiitwi Bin Swabrah (ALLAAH Amridhi!):

“Pandisha sana maji puani ila usifanye hivyo ukiwa umefunga”.

Ina maana mtu akiwa na swaumu achunge juu ya kupandisha sana maji puani bali atapandisha wastani ili yasimpenye kwenye kooni.

Rej “Sunan Abiy Daud No 142/  Tirmidhiy No 788”.

والله ولي التوفيق.

Muhusika: duaatsalaftz

Chanzo: www.duaatsalaftz.net

Imehaririwa: 22/10/2016