Makala

Ukombozi Wa (Allāh) Mneemeshaji Katika Kumjibu Mshia Muovu – 01

Star InactiveStar InactiveStar InactiveStar InactiveStar Inactive
 

UTANGULI:

Sifa njema zote anastahiki Allāh Mola wa walimwengu wote, Mwenyekumiliki Siku ya Malipo, ambaye ni Yeye tu ndiye tunayemwabudu

na Yeye tu ndiye tunayemwomba msaada.

Swala na salamu zilizokamili zimshukie Nabii wetu na Mtume wetu Muhammad bin ‘Abdillāh, pamoja na Swahaba zake na Aali zake.

Huu ni mwanzo mzuri utakaokuwa na mwendelezo mzuri pia kwa idhini ya Mola mkarimu katika kutoa majibu ya kijitabu kilichoandikwa na mshia Ayatollah Sayyid Sadiq Mahdi Husaini Al-Shiiraaziy, alichokiita “Haqāiqu ‘An Shii’ah”, na kufanyiwa tarjamah kwa lugha ya kiswahili na aliyeitwa na babiye: Abdul-Karim Juma Nkusui, na kuchapishwa na Sayed Al-Shohadaa Charitable Committee (ya Kuwait), kilichopewa jina kwa lugha ya kiswahili “UKWELI WA SHIA”, na haki yake kilipaswa kiitwe “UWONGO WA SHIA”.

Kijitabu hiki, nilimuona nacho mmoja katika ndugu akiwa amekihifadhi katika maktaba yake ya nyumbani, baada ya kumhoji kulikoni na hiki kitabu cha shia!! Akajibu kuwa wanapewa vijitabu kama hivyo na mfano wake makazini mwao, ndipo nilipompokonya na badala yake nikampa kitabu ambacho kitakuwa na manufaa naye, ni katika ule mlango wa mpokonye mwana kiwembe na badala yake umpe pipi.

Likiwa lengo letu kuu ni kuipa jamii elimu na kumjuza asiyejua juu ya talbisi na udanganyifu ufanywao na Shia Ithnay-Ashariyyah, kwa lengo lao lile lile la kuwatia mitegoni Ahlus-Sunnah Wal-Jamā’ah na kuwateka katika nyavu zao na malema yao bid’ah na talbiis.

Kisha elewa ndugu msomaji ya kwamba sisi tumechukua ahadi katika nafsi zetu kwamba tutajitaahidi kuchunga ukweli na uadilifu katika nukulu zetu, pamoja na chuki zetu kuuchukia ushia na mashia (na tunataraji malipo kutoka kwa Allāh juu ya hili) hatuhalalishi tendo la kuwanasibishia yasiyo yao katika maneno, au kuwasifu kwa wasiyokuwa nayo katika matendo.

Na hilo ni kwa sababu kuu mbili:

  1. Kama kweli kujishughulisha kwetu na jambo hili la kuwajibu (radd) watu waliokwenda kinyume lengo lake ni kutafuta radhi za Allāh, haitokuwa sawa kabisa kutumia njia za urongo dhulma na udanganyifu, kwani mambo hayo ni katika makubwa yamchukizayo Allāh Subhānah, na kumweka mbali mja na Mola wake.
  2.  Dini ya Allāh Allāh Allāh hunusuriwa kwa haki na uadilifu, na wapitao katika njia za urongo na talbiis ni watu wa batili siku zote, wale ambao wameshindwa kuzipata hoja na dalili za kisharia kutetea madhehebu zao.

Na majibu yetu haya tumeyaita:

“Fat-hul-Mun’im Fir-Radd ‘Alal-Rāfidhiyy Al-Mujrim”

Kwa maana:

“Ukombozi wa (Allāh) Mneemeshaji katika kumjibu mshia muovu.”

Na mwendo wetu katika njia ya majibu hautokuwa wa kasi kwani wanasema mwendo wa kasi unaua, mwendo wetu ni wasaa wetu tulionao, unaweza ukawa wa kobe au wa kinyonga.

Twamuomba Allāh atuwafikishe katika amali yetu hii, na aturuzuku Ikhlasi katika kauli na amali, na aijaalie kazi hii iwe kwa ajili ya kupata radhi zake, na aziepushie dhamira zetu hadhi za kilimwengu.

 

 

Mhusika: Al-Akh Abuu Ayman Al-Shiraaziy
Mkusanyaji: http://duaatsalaftz.net/

Nasaha

©2020 uaat Salaf Tanzania - . All Rights Reserved. Designed By Wajanjatech.Com

Search