Makala

Ukombozi Wa (Allāh) Mneemeshaji Katika Kumjibu Mshia Muovu – 03

Star InactiveStar InactiveStar InactiveStar InactiveStar Inactive
 

Neno la Mchapishaji limenena:

“Baadhi ya Waislamu huwalaumu wenzao kwa baadhi ya matendo wanayoyafanya na kuyaona kuwa sio ya Kiislamu, hivyo, kuwakufrisha kwayo na kuwatenga
bila kujua kwamba hizo ni mbinu za maadui wasioutakia mema Uislamu.”

Majibu Yetu:

Yalaiti angelitutajia mfano mmoja wa baadhi ya hao Waislamu ili tuondokewe na gagaziko hili!! Yalaiti angelitutajia pia mfano mmoja wa hayo matendo ambayo yanaonekana kuwa si ya Kiilslamu! Lakini watu wa batili siku zote maneno yao huwa katika mifundo hayawi nyoofu.
Alafu tendo kuwa la Kiislamu au si la Kiislamu mizani yake sahihi ya kulipima hilo ni Uislamu wenyewe, kwani yako mengi ya matendo wenye matendo hayo wanayahesabu kuwa yapo katika Uislamu na wanasubiri huko umuri Kiyama malipo makubwa kutoka kwa Mola wao ilhali ukiutazama Uislamu wenyewe unayakataa, sasa suala la kuona kuwa hili ni la Kiislamu au si la Kiislamu, hili halipo katika maono na rai za watu, kwamba lile watakaloliona watu fulani lipo katika Uislamu waachwe nalo hata kama Uislamu umelipinga na kulikataa, na lile ambalo lipo katika Uislamu kwa kuwa watu fulani hawalitaki wala hawalipendi litolewe katika Uislamu, hapana, sivyo hivi mambo yanavyoendeshwa.
Hakkak katika tunayoamini ni kuwa matendo ya kufuru yapo, na yanatoa watu katika Dini, na hili lipo katika Dini zote hata katika Dini ya Ushia, yako mambo shia akiyafanya basi ametoka katika ushia wake, kama vile kuacha kuamini juu ya taqiyyah, bali kufuru zipo hata kwenye uyahudi na unaswara, kwa maana lipo jambo ukilifanya unahukumiwa kuwa umetoka katika Dini yako, sawa sawa iwe Dini hiyo ni ya haki kama vile Uislamu, au ya batili kama vile ushia na uyahudi.
Kufru kwetu sisi Waislamu imegawika katika makundi makuu mawili kwa mujibu wa nususi za Kisharia:
  1. Kufru ikufurishayo (kufru kubwa).
  2.  Kufru inayotia katika ufasiki (kufru ndogo).
Kwa maana ipo ambayo inamtumbukiza mtu katika dimbwi la ukafiri na kumtoa katika mila ya Kiislamu, na ambayo haimtumbikizi katika dimbwi hilo bali humtupa katika shimo la ufasiki.
Wa kwanza akawa ni kafiri, na huyu wapili akawa ni Muislamu mpungufu wa Iymani.
Japo inatakikana ieleweke kuwa, suala la kukufurisha halijaegemezwa kwa mtu, kwamba amkufurishe amchukiaye na ampe Uislamu ampendaye, bali marejeo ya jambo hilo ni kwa Allāh Mtukufu na Mtume wake Muhammadﷺ, kwani jambo hilo lipo katika hukumu za kisharia ambazo hurejeshwa kwenye Kitabu cha Allāh na Sunnah za Mtume Muhammadﷺ, hivyo hakufurishwi ila yule ambaye dalili zimesimama juu ya ukafiri wake.
Ifahamike kuwa jambo la asili kwa kila Muislamu ni kubakia katika Uislamu wake na uadilifu wake mpaka upatikane uhakika wa kuondokewa na kimoja katika hivyo viwili au vyote kwa pamoja na kwa dalili za Kisharia.
hivyo, haitofaa kuzembea katika kukufurisha watu kwani atakayefanya hilo kuna hatari ya kukabiliwa na mambo makubwa mawili ya hatari:
1) kumzulia Allāh katika hukumu aliyoitoa kwa yule aliyemkufurisha kwa dhulma.
Na katika hili anasema Ibn Al-Qayyim:
“Elewa ewe Mufty ya kwamba wewe unatia saini kwa niaba ya Allāh huku aridhini.”
Rejea: “إعلام الموقعين”.
sasa ole wake mtu katika Fatawa zake na kukufurisha kwake.
2) kutumbukia katika hilo shimo alilomtumbukiza nduguye.
Na katika hili la mwisho, imeswihi hadithi ya Mtukufu Mtume Muhammadﷺ kwamba amesema:
“Atakapomkufurisha mtu nduguye, basi tayari ukafiri umemuangukia mmoja wao, kama atakuwa amepatia (ni afadhali) na kinyume chake ukafiri utamrudia yeye mwenyewe.”
Bukhari (6104) na Muslim (60).
Na Wanazuoni wetu wa Kiislamu wanatoa tahadhari kubwa sana katika mlango huu wa kukufurishana, na wanasema kabla ya kutoa hukumu hii ni lazima mtu ayaangalie kwa umakini mambo mawili:
  1.  Kujulisha kwa Kitabu na Sunnah kuwa kauli (hii) au tendo (hili) hukufurisha, na sio kwa matashi ya mtu.
  2.  kuwezekana kwa kuanguka hukumu hiyo ya “ukafiri” kwa huyo aliyefanya (hilo jambo) au aliyelisema hilo neo.
Kwa maana, hata kama amefanya jambo la ukafiri au amesema neno la ukafiri haifai kumkufurisha mpaka yatimie kwake masharti na vimuondoke vizuizi.
Mfano wa masharti hayo ni:
(a) awe anajua kuwa afanyalo au asemalo ni jambo lenye kumkufurisha mtu.
Kinyume chake ni yeye kuwa mjinga wa hilo, sasa mtu kama huyu ambaye ni jaahil huna ruhusa ya kumkufurisha, na zimekuja dalili nyingi katika Qur’an juu ya jambo hili la kutotiwa makosani asiyejua.
Mfano:
Anasema Allāh katika Kitabu Kitukufu:

وَمَا كَانَ اللَّهُ لِيُضِلَّ قَوْمًا بَعْدَ إِذْ هَدَاهُمْ حَتَّىٰ يُبَيِّنَ لَهُم مَّا يَتَّقُونَ ۚ ” التوبة (١١٥).

“Na haiwi kwa Allāh kuwahisabu watu kuwa wamepotea baada ya kuwa Amewaongoza mpaka Awabainishie ya kujiepusha nayo.”
Kama hawajabainishiwa ya kujiepusha nayo watakapoyafanya hawana hatia.
At-Tawbah (115).
Na amesema:

وَمَا كَانَ رَبُّكَ مُهْلِكَ الْقُرَىٰ حَتَّىٰ يَبْعَثَ فِي أُمِّهَا رَسُولًا يَتْلُو عَلَيْهِمْ آيَاتِنَا ۚ” القصص (٥٩).

“Na Mola wako haangamizi miji mpaka Ampeleke Mtume katika mji wao mkuu, awasomee Aya Zetu.”
Hakuna kuangamizwa kabla ya ujumbe wa Allāh kufika.
Al-Qasas (59).
Na amesema:

وَمَن يُشَاقِقِ الرَّسُولَ مِن بَعْدِ مَا تَبَيَّنَ لَهُ الْهُدَىٰ وَيَتَّبِعْ غَيْرَ سَبِيلِ الْمُؤْمِنِينَ نُوَلِّهِ مَا تَوَلَّىٰ وَنُصْلِهِ جَهَنَّمَ ۖ وَسَاءَتْ مَصِيرًا” النساء (١١٥).

“Na atakayemwasi Mtume baada ya kumdhihirikia uwongofu na akafuata njia isiyokuwa ya Waislamu, Tutamgeuza alikogeukia mwenyewe na Tutamwingiza katika Jahanamu, napo ni pahali pabaya kabisa mtu kurudia.”
Atatiwa motoni kwenye marejeo mabaya kwa kumkhalifu Mtume (swalla Llāhu alayhi wasallam), na baada ya kubainikiwa na elimu.

 

An-Nisa (115).

Na kwa kipengele hiki ndio maana wakasema Wanazuoni ya kuwa:
“hatokuwa kafiri anayepinga mambo ya faradhi katika Uislamu pindi akiwa ni mgeni katika Uislamu mpaka pale atakapobainishiwa akajua.”
Hivyo jambo la kukufurisha halikataliwi moja kwa moja, wala halikubaliwi moja kwa moja, na kwamba marejeo yake ni Kitabu na Sunnah, atakufurishwa aliyekufurishwa na Allāh na Mtume wake (swalla Llāhu alayhi wasallam), kwa vigezo ambavyo tumekiashiria kimoja wapo.
Na kukufurishwa kwenu nyie shia masharti yametimu na vizuizi vimetoweka.
Sasa kauli yenu hii imelenga kuwaziba midomo Ahlus-Sunnah dhidi ya kufru mlizokuwa nazo, mkaona mujiwekee ngome na kujificha kwenye kivuli cha Waislamu ilhali nyinyi na Uislamu ni mbingu na ardhi.
Mnataka pale mnapowatukana Maswahaba wa Mtume wetu (swalla Llāhu alayhi wasallam) na kuwakufurisha muachiwe?
Mnataka pale mnapomtuhumu zinaa mama wa Waislamu Aisha kipenzi cha Mtume wetu (swalla Llāhu alayhi wasallam, na radhi za Allāh ziwe juu yake) msisemwe?
Mnataka pale mnapotangaza itikadi zenu za ukafiri kuwa Maimamu wenu wamefika katika daraja ambalo hakuweza kulifika Nabii Muhammad (swalla Llāhu alayhi wasallam) wala Malaika Jibriil (‘alayhis-Salaam), mnyamaziwe?
Mnataka pale mnapowaeleza Waislamu kuwa Maimamu wenu wanajua elimu ya ghaibu, mkampora Allāh muumba wa mbingu na ‘Arshi tukufu, sifa yake hiyo aliyopwekeka nayo, musifiwe?

الرافضة في الأرض مرفوضة
واجب علينا الكل نرفضها
قد سببت في أرضنا الفوضى.

Na tukizungumzia suala la kutenga watu, tunaona kuwa hili ni jambo ambalo lipo kisharia zaidi, kwani ni Mtume Muhammadﷺ na Maswahaba zake walilifanya hilo, kwa maana waliwatenga baadhi ya ndugu zao kama vile K’ab bin Mālik, Hilāl bin Umayyah, Murārah bin Rabii (Allāh awaridhie).
hivyo ni jambo ambalo halina shaka ndani yake kuwa lipo katika Dini yetu ya Kiislamu, na hufanyiwa mtu anayedhihirisha uasi kwa lengo la kumsaidia kumrejesha katika utiifu, kwa vidhibiti walivyovitaja Wanazuoni, hivyo kuliita tendo hili la kisharia kuwa ni mbinu za maadui hamuoni kuwa mnatutukania Mtume wetu (swalla Llāhu alayhi wasallam), na kumtuhumu kuwa ameingiza katika Dini yetu mbinu chafu za maadui wasioutakia mema Uislamu!?

رمتني بدائها وانسلت

sasa hatolopinga hili ila mtu mwenye maradhi mithili yenu.
Lakini kabla ya kuchukuliwa kwa hatua hii kwa mkosaji, kwanza kabisa hunasihiwa na kubainishiwa, kwamba (mathalan) jambo hili ni bid’ah, au ni jambo la haramu kwa ushahidi kadhaa wa kadhaa, usilifanye. Kama atakubali nasaha na kuliacha basi hapo huhimidiwa Allāh na kushukuriwa, na kama ataendelea baada ya kubainishiwa hapo ndipo anapotengwa mpaka pale atakapokoma na kurudi kwa Mola wake kwa toba ya kweli.
Pamoja ya kwamba katika kumtenga huko kuna maslahi na mafsad ambayo yatachungwa.

 

وهجران من أبدى المعصية سنة

وقد قيل إن يردعه أوجب وأكد

Anatengwa mtu kwa ajili ya Allāh, pale itakapokuwa kuna maslahi yatakayopatikana kwa mtengwaji na mtengaji na jamii.
Mfano wa maslahi kwa mtengaji:
Ni pale atakapobainikiwa kuwa kujenga kwake ukaribu na mzushi fulani kutamtoa katika Dini na msimamo wa haki na kumpeleka katika upotevu, mithili ya Sunniy kusuhubiana na shia.
Kama ndugu msomaji utakuwa na kumbukumbu nzuri utaungana nami kuwa ushia zamani hapa nchini ulikuwa ni wa wahindi tu, na walikuwa ni wachache wenye aibu katika kuendesha yale maandamano yao yamwezi wa Muharram, na walikuwa zamani wakitembea usiku kwa aibu, leo hii mpaka magolo nao wamegeuka kuwa ni shia, na wanafanya maandamano yao ya Muharram mchana kweupe, na ukichungunza kwa makini hawa viongozi wa shia golo (weusi) wote walikuwa ni wasunny waliozaliwa na wazazi wao Usilamuni, na kusoma kwa Masheikh wa Kishaafiy, baadhi yao walikuwa ni wanafunzi wa Sheikh Muhammad bin Sheikh Ayoub Al-Kamaadhiy ( غفر الله له), kilichowaghuri ni kitu gani? Ni pale walipoutupilia mbali msingi huu wa kuwatenga watu wazushi na waovu, wakaingia ushiani wakautupa Usunny waliozaliwa nao na wazazi wao, tangu alipokuwa mtu akimtaja Abūbakr na ‘Umar na kuwatakia radhi za Allāh, mpaka kufikia leo hii wakiwataja na kuwatakia laana.

قد كان ما خشينا أن يكونا
إنا إلى الله لراجعونا

Mfano wa maslahi kwa jamii ya Waislamu:
Ni pale Sheikh anayeaminika anapoonekana anaingia na kutoka na mzushi, anacheka naye na kuhadithi, anakula naye anapanda naye na kushuka, anahudhuria katika hafla zake nk.
Hapo jamii ya Waislamu bila shaka itadhurika kwa sababu ya Sheikh huyo wanayemuheshimu na kumwamini pale wanapomuona amekamatana barabbara na mzushi huyo. Wataona kuwa yanayofanywa na huyo mzushi si mabaya, kwani mbona Sheikh fulani yupo naye? Kama angekuwa hafai basi Sheikh wetu asingeongozana naye!
Hapo utaona umuhimu wa nafasi ya msingi huu wa kuwatenga wazushi na waharibifu wa Dini.
Na alhamdulillah tumepata kusikia Sheikh mmoja mkubwa hapa jijini (Dar-Es-Salaam) ambaye anawakumbatia wazushi na waovu, alipita mbele kutaka kuswalisha Msikiti fulani, Waislamu wanaokerwa na hali yake hiyo walikatika safuni, na huu ni mwanzo wa kheri kuona kuwa Waislamu wa Sunniy sasa wanayaelewa mambo, wanawajua sasa ni akina nani watu wa maslahi ambao hawana itikadi wanayoitetea zaidi ya kutazama jinsi ya kujaza matumbo yao.

 

Mhusika: Al-Akh Abuu Ayman Al-Shiraaziy
Mkusanyaji: http://duaatsalaftz.net/

Nasaha

©2020 uaat Salaf Tanzania - . All Rights Reserved. Designed By Wajanjatech.Com

Search