Je Kushika Tupu Kunatengua Udhu?


Swali:
Assalamu Alaykum
Naomba kufahamu ni ipi kauli yenye nguvu zaidi kuhusu kushika utupu kuwa kunatengua au hakutengui udhu ?? maana kuna hadithi mbili moja inasema hicho nikiungo kama viungo vyengine na nyengine inabainisha kuwa Atakae Shika utupu akatie udhu tena
naomba kufahamu kwa dalili ni ipi kauli sahihi zaidi ?
Jawabu:

وعليكم السلام ورحمة الله وبركاته.
الحمد لله رب العالمين، والصلاة والسلام على أشرف الأنبياء وإمام المرسلين ، نبينا محمد وآله وصحبه وسلم.
Kwa hakika ni jambo lenye ikhtilafu za Wanazuoni wetu wa Kiislamu tangu zamani mpaka leo hii
Na sababu kuu iliyopelekea kupatikana kwa tofauti hizo ni hadithi mbili ulizozitaja kwa lugha ya jumla katika maelezo ya swali lako.
Hadhithi ya kwanza ni hadithi ya swahaba Busrah Bint Swaf’waan (ALLAAH Amridhi!), kwamba amesema Mtume (swalla LLAAHU ‘alayhi wasallam):
“من مس ذكره فلا يصل حتى يتوضأ” روه أحمد وأبو داود.
“Yeyote atakayegusa dhakari yake basi asiswali mpaka achukue udhu”. Ameipokea Ahmad na Abuu Daud
Na hadithi ya pili ni hadithi ya swahaba twalqi Bin ‘Aliyy (ALLAAH Amridhi!), kwamba alikuja bedui kumuuliza Mtume (swalla LLAAHU ‘alayhi wasallam) kuhusu udhu wa aliyeshika dhakari yake, akasema Mtume (swalla LLAAHU ‘alayhi wasallam) :
“وهل هو إلا بضعة منك” أبو داود
Na haikuwa hiyo (dhakari) ila ni sehemu ya viungo vyako. Ameisahihisha Al-Albaaniy (ALLAAH Yarhamhu
Hizo ndizo hadithi mbili tegemewa katika masuala hayo.
Tofauti zimekuja kuanzia kwa Maswahaba (ALLAAH Awaridhi!), mpaka maimamu wa Kitaabiina na waliokuja baada yao miongoni mwa Maimamu wakuu wa madhehebu (ALLAAH Awarham wote!).
Baina ya mwenye kusema hadithi ya Twalqi Bin ‘Aliyy imetangulia kabla ya Mtume (swalla LLAAHU ‘alayhi wasallam) kuisema hadithi ya Busrah Bint Swaf’waan.
Hivyo wakadai kuwa hadithi ya Twalqi isemayo kuwa dhakarni kiungo tu katika mwili imefutwa kwa hadithi ya Busrah isemayo yeyote atakayegusa dhakari yake basi asiswali mpaka achukue udhu.
Na wale ambao wameidhoofisha kabisa hadithi ya Twalqi Bin ‘Aliyy (ALLAAH Amridhi!).
Lakini baadhi ya ‘Ulamaa wetu wakarimu (ALLAAH Awarhamu!), wanaonelea kuwa zote mbili ni hadithi sahihi na hivyo kufanyiwa tawfiiq baina yake ni jambo la wajibu kuliko kudai udhaifu au moja kuifuta nyengine.
Na hayo ameyataja Ibn ‘Uthaymiin (ALLAAH Amraham!) katika sharh buluugh na al-usuul min-‘ilmil-usuul
Kwahiyo yeye akaenda na kauli ya kuwa atakayegusa dhakari yake kwa matamanio huyo ni wajibu kwake kuchukua udhu.
Na ambaye hajagusa kwa matamanio ni sunnah kwake kufanya hivyo (kuchukua udhu).
Na hivyo ndivyo alivyozijumuisha hadithi mbili hizo ambazo kwa mtazamo wa mbali zinakhtalifiana.
Na kwakua zote amezisahihisha Al-Imaam Al-Albaaniy (ALLAAH Amrahamu!), moja katika al-ir-waa (ambayo ni hadithi ya Busrah), na nyengine katika sahiihi abiy Daud ambayo ni hadithi ya Twalqi bin ‘Aliyy, alisema hivi katika kuzijumuisha:
وإن كان المس بدون شهوة فوضوءه لا ينقض ، لأنه يكون كما لو مس بضعة أخرى من بدنه، وإن كان المس بشهوة، فالعمل على حديث بسرة، ولا يخالفه هذا، لأنه لا يكون المس حينئذ كما لو مس بضعة أخرى
Ikiwa kugusa bila ya matamanio basi udhu wake hautenguki kwasababu ni sawa na kugusa kiungo chengine katika mwili wake
Na kama kugusa kutakuwa kwa matamanio basi ifanyiwe kazi hadithi ya Busrah, na wala haitopingana na hadithi hii (ya Twalqi), kwasababu ugusaji huu (wa shah-wah) hautokuwa sawa na ugusaji wa kiungo chengine (kinachoguswa bila ya shah-wah, kama vile pua,mdomo nk) sahiih Abiy Daud 1/334.
Na wapo miongoni mwa Wanazuoni ambao wanaichukua hadithi ya Busrah juu ya usunnah na kuibeba hadithi ya Twalqi juu ya kukana uwajibu.
Amesema Ibn Taymiyyah (ALLAAH Amraham!):
والأظهر أيضا أن الوضوء من مس الذكر مستحب لا واجب، وهكذا صرح به الإمام أحمد في إحدى الروايتين عنه، وبهذا تجتمع الأحاديث والآثار بحمل الأمر به على الإستحباب ليس في نسخ قوله (وهل هو إلا بضعة منك)، وحمل الأمر على الإستحباب أولى من النسخ
Na vile vile kinachodhihiri, ni kuwa udhu wa aliyegusa dhakari ni sunnah si wajibu. Na hivi ndivyo alivyozungumza kwa uwazi Imam Ahmad katika moja ya riwaya zake mbili.
Na kwa kauli hii zitajumuika hadithi na aathaari , kwa kuichukulia amri (ya kuchukua udhu kwa aliyeshika dhakari kuwa ni sunnah na wala haikuja kufuta hadithi haikuwa hiyo ila ni sehemu katika maungo yako.
Na kuichukulia amri hiyo juu ya sunnah ni bora kuliko madai ya kufuta (21/ 241).
Hizi ni baadhi ha kauli za baadhi ya Wanazuoni wetu (ALLAAH Awarham!) na ndio kauli yenye nguvu kwa mwandishi.
والعلم عند الله
Sanjari na hilo lililopita ni haya hapa
kugusa dhakari kwa hali ya kusahau:
Aliyegusa dhakari yake kwa kusahau au kutodhamira udhu wake pia unachenguka ni sawa na kuigusa kwa makusudi hakuna tofauti katika hilo kwa kuenea kwa hadithi.
Na hii ameisema Al-Awzaa’iyy, Al-Shaafi’iyy, Is-haaq, Ahmad na Abuu Thawr (ALLAAH Awarham!)
Rej: [al-awswat 1/193, al-maj’muu 2/34, al-mughniy 1/242].
kugusa dhakari kwa mgongo wa kiganja:
Hakuna tofauti baina ya juu ya kiganja na tumbo la kiganja katika kuigusa dhakari, na kwamba yote hayo hutengua udhu. Na Kwasababu ya kuenea (‘umuum) kwa hadithi ya Busrah.
Na hili amelisema Imam ‘Atwaa bin Abiy Rabaah, Al-Awzaa’iyy, Ahmad, ama Imam Maalik ,Al-Shaafi’iyy na Is-haaq wao wamelikhusisha la kutenguka kwa udhu pale atakapojishika kwa tumbo la kiganja (tu!).
Na kauli yenye nguvu ni kutotofautisha kwa juu ya kiganja wala kwa tumbo lake.
Rej: [al-sharh al-mumti’i 1/320].
kugusa dhakari kwa muundi wa mkono (dhiraa):
Kugusa dhakari kwa dhiraa hakutengui udhu.
Na hii ni kauli ya Imam Malik, Allayth bin Sa’ad, Al-Shaafi’iyy na Ahmad.
Kwasababu hukumu ya kutenguka kwa udhu imefungamanishwa na kiganja tu.
Rej: [ al-sharh al-mumti’i 1/320 , al-awswat 1/208].
kugusa dhakari juu ya kizuizi:
Hili halitengui udhu, kwani hili halihesabiki kuwa linaingia kwenye ugusaji unaokusudiwa wa ngozi kwa ngozi.
Na hili amelirajihisha Ibn ‘Uthaymiin (ALLAAH Amraham!).
Rej: [al-sharh al-mumti’i 1/320]
kuigusa dhakari ya mtu mwengine:
Kugusa dhakari ya mtu hilo halitengui udhu, awe huyo aliyeguswa dhakari yake ni mtumzima, mtoto mdogo, hai au mfu.
Na katika hili wameliendea akina:
Imam Malik,Daud, na imerajihishwa kauli hii na Imam Ibn Hazm na Ibn ‘Abdil-barr.
Kwasababu dalili imemtaja na kumkusudia atakayejishija dhakari yake (tu!).
Rej: [al-mughniy 1/243].
udhu wa aliyeshikwa dhakari yake:
Aliyeshikwa dhakari yake hautenguki udhu wake katika madh-hab sahihi za Wanazuoni, kwasababu ugusaji haujatokea kwake.
Na hii ni kauli ya Al-Shaafi’iyy na Ahmad.
Rej: [ al-majmuu 2/41].
mwanamke kugusa utupu wake wa mbele:
Hutenguka udhu wake, kwa ushahidi wa hadithi ya Busrah Bint Swaf’waan , na hadithi Amri bin Shu’ayb kutoka kwa baba yake kutoka kwa babu yake , kutoka kwa Mtume (swalla LLAAHU ‘alayhi wasallam) amesema:
وأيما امرأة مست فرجها فلتتوضأ أخرجه أحمد وإسناده حسن
Na mwanamke yeyote atakayejishika tupu yake ya mbele basi na atawadhe
kugusa utupu wa nyuma:
Kujigusa duburi hakutengui udhu.
Na kwa hili ameliendea Imam Malik na watu wa rai, na pia ni riwaya moja iliyopokelewa kutoka kwa Imam Ahmad na Sufyaan Al-Thawriyy na Qataadah .
Na ni kauli yenye nguvu kwakuwa hakuna dalili juu ya hili.
Rej: [al-sharh al-mumti’i 1/336].
kugusa tupu ya mnyama:
Jopo la walio wengi miongoni mwa Wanazuoni wanaonelea kuwa kugusa utupu wa mnyama hakubatilishi udhu , awe mnyama huyo ni twahara au najisi kwakukosekana dalili juu ya hilo.
Amesema Imam Al-Nawawiyy (ALLAAH Amraham!):
لا ينقض وضوء من مس فرج البهيمة عندنا وبه قال العلماء كافة إلا عطاء والليث بن سعد
Hautenguki udhu wa mwenye kugusa tupu ya mnyama kwetu sisi (shaafiiyyah), na kwa kauli hii wamesema ‘Ulamaa wote, ila ‘Atwaa na Allayth bin Sa’ad”. [al-majmuu 2/43]
mwenye tupu mbili (kunthaa) kugusa tupu zake
Akigusa tupu zote mbili basi umetenguka udhu wake.
Na kama ataigusa moja hautenguki kwa kupatikana ihtimali ya kuigusa ile iliyozidi, na yakini ya twahara haiondoki ila kwa yakini.
Na akigusa moja kisha akagusa yapili pia hana udhu.
Rej: [al-mughniy 1/245].
والله ولي التوفيق
Muhusika: duaatsalaftz
Chanzo: www.duaatsalaftz.net
Imehaririwa: 27/01/2017