Je Yafaa Kumrekebisha Imam Akikosea Katika Swala?


Swali:
ikiwa imaam amekosea kusoma mfano ktk surat tiin ktk neno الإنسان badala ya kulinasibisha yeye akalirufaisha je ni lazima anaefahamu ya kuwa imamu amekosea amrekebishe au ni mustahabu?
Kama ni lazima kumrekebisha vipi kwa yule ambaye anakhofia kumrekebisha kwa kuogopa ya kwamba watu watasema anajiona afahamu sana kila kosa amrekebisha imam?
Baaraka Llaahu fiykum
Jawabu:
وعليكم السلام ورحمة الله وبركاته.
الحمد لله رب العالمين ، والصلاة والسلام على رسول الله محمد بن عبدالله وآله وصحبه.
Kilicho sahihi katika maneno ya Wanazuoni ni kuwa yafaa kumzindua Imam pale anaposahau aayah au kuitamka herufi kimakosa, na wakawajibisha hilo katika suuratul-faatiha.
Kwa ushahidi wa riwaya ya Imam Ahmad na Abuu Daud (ALLAAH Awarham!):
“Kwamba hakika Mtume (swalla LLAAHU ‘alayhi wasallam) aliswalisha siku moja akasahau kuisoma aayah. (baada ya swala kuisha) swahaba mmoja alimwambia :
“Ewe Mtume wa ALLAAH! Kuna aayah hii na aayah hii!?”
Akasema Mtume (swalla LLAAHU ‘alayhi wasallam):
“Kwanini usingenikumbusha!?”. Ameihasanisha Imam Al-Albaaniy (ALLAAH Amraham!) katika “Al-Swahiihah 802”.
Na imekuja riwaya kutoka kwa Abuu Daud (ALLAAH Amraham!) kutoka kwa Ibn ‘Umar (ALLAAH Awaridhi):
“Kwamba Mtume (swalla LLAAHU ‘alayhi wasallam) , aliswalisha swala (fulani) akachanganya. Baada ya kumaliza swala alimwambia Ubayy Ibn Ka’ab (ALLAAH Amridhi!):
“Je umeswali nasi (leo hii!)”.
Akajibu:
“Ndio”.
Akasema :
“Kipi kimekuzuilia (usituzindue!?”. Ameihasanisha Al-Imaam Al-Albaaniy (ALLAAH Amraham!) katika “Al-Swahiiha No 803”.
Na amepokea Imam Al-Bayhaqiyy (ALLAAH Amraham!) , kutoka kwa Aliyy bin Abiy Twaalib (ALLAAH Amridhi!) kwamba amesema : “Atakapokuhitaji chakula Imam basi mpe”. yaani ukihisi anahitaji kumzindua mzindue .
Ila ambacho mtu anatakiwa kukifahamu ni kuwa haitakikani kuwa na papara wakati wa kumzindua imam kwa aayah aliyoisahau au kwa aayah aliyoikosea kwani huenda mwenyewe akatanabahi na kujirekebisha.
Pia haijuzu kwa ambaye atamsahihisha Imaam awe na haraka kufanya hivyo ila atakapokuwa ana thiqa na hifdhi yake asije akawa yeye ndo mwenye kosa.
Ama kukhofia kumtanabahisha Imaam kwa dhana ya kuwa watu watamdhania kwamba yeye anajiona hiyo ni fikra ya kishaytwani anayemtia wasi wasi . Asisite kumtanabahisha wala asione haya kwani haya kwa mazingira kama hayo haihimidiwi.
والله ولي التوفيق
Muhusika: duaatsalaftz
Chanzo: www.duaatsalaftz.net
Imehaririwa: 09/12/2016