KHATARI YA KUKOPA (MADENI)!!


Hakika imekuja Shari’ah ya Kiislamu kwa makemeo makali sana kunako suala la madeni.

Na kumtaka Muislamu ajitaahid kadri ya uwezo wake kuachana na tabia hiyo ambayo katika athari zake ni mtu kuwa dhalili kwa aliyemkopa nk.

Imepokelewa kutoka kwa ‘Aaisha (ALLAAH Amridhi!) , kwamba Mtume (swalla Llaahu ‘alayhi wasallam) alikuwa akiomba dua katika swala zake:

“Ewe ALLAAH, hakika mimi najilinda kwako kutokana na madhambi na madeni”

Akaulizwa na bwana mmoja,  “mara nyingi unasikika kujilinda (kwa Allaah) kutokana na madeni!”  akasema Mtume (swalla LLAAHU ‘alayhi wasallam):

“hakika mtu akiwa na madeni huzungumza uongo na kuahidi bila ya kutekeleza”.   Bukhariy (832) Muslim (589).

Na imepokelewa kutoka kwa Muhammad bin Jahshi (ALLAAH Amridhi!) amesema:

“Tulikuwa tumekaa mbele ya Mtume (swalla LLAAHU ‘alayhi wasallam) , mara akainua kichwa chake kutazama mbinguni kisha akaweka mkono wake juu ya paji lake la uso kisha akasema:

“Utakasifu ni wa ALLAAH! makemeo makubwa kiasi gani yaliyoshushwa (leo!)”

Tukanyamaza kisha tukaondoka, ilipofika siku ya pili nilimuuliza,
Ewe Mtume wa ALLAAH , ni yapi hayo makemeo yaliyoshushwa!?

Akasema:

“Na apa kwa yule ambaye nafsi yangu imikononi mwake!  Lau ikitokea mtu atauwawa kwenye jihadi kisha akahuyishwa kisha akauwawa tena na kuhuyishwa kisha akauwawa tena ilhali ana deni hataingia peponi mpaka alipiwe deni lake”  Nasaaiyy (4605) na ameihasanisha Al-Imaam Al-Albaaniy (ALLAAH Amraham!).

Sambamba na hadithi hiyo, nimesema mimi (Al-Shiiraaziy Allaah anisamehe!) : “Amemtaja hapo Mujaahid , na fadhila ambazo tunazijua kwa watakaopata shahada katika jihaadi ni nyingi, kama vile kutoulizwa maswali makaburini, kupewa ofa ya kuwaombea ndugu zao na jamaaa watu sabini ambao wamehukumiwa moto, lakini  deni lina khabari kubwa”.

Na imesihi hadithi kuwa Mtume (swalla LLAAHU ‘alayhi wasallam) ameacha kumswalia shahaba kwakuwa alikufa na deni , mpaka pale swahaba Abuu Qataadha alipolibeba mbele ya Mtume (swalla LLAAHU ‘alayhi wasallam) deni la nduguye  ndipo alipomswalia.

Na alipokutana naye siku ya pili alimpasha khabari kuwa deni alishalilipa.

Akasema Mtume (swalla LLAAHU ‘alayhi wasallam):

“Sasa hivi ndiyo ngozi ya mwili wake imeanza kupoa”. Ahmad katika Musnad na ameihasanisha hadithi hii Al-Imaam Al-Nawawiyy kwenye “Al-Khulaaswah” na ameitaja Al-Albaaniy katika “Al-Ahkaam”.

Amesema Al-Haafidh (Allaah Amraham!) katika fat’h :

“Na katika faida za hadithi hii kuna kujulishwa kuwa haipasi mtu kuwa na deni kwasababu ya ugumu na uzito wa jambo hili, isipokuwa mtu akidharurika”.

Na imepokelewa kutoka kwa Thawbaani Mawlaa wa  Rasuul (Swalla Llaahu ‘alayhi wasallam) amesema,

Amesema Mtume (swalla LLAAHU ‘alayhi wasallam) :

“Yeyote atakayekufa ilhali yupo mbali na mambo matatu

1. Kiburi.
2. Wizi wa ngawira.
3. Madeni.

Ataingia peponi”.  Al-Tirmidhiy (1572)  na ameisahihisha Al-Albaaniy (ALLAAH Amraham!).

Na inswafu waliyokuwa nayo Maswahaba wa Mtume wetu (swalla LLAAHU ‘alayhi wasallam/ na radhi za ALLAAH ziwe juu yao) ni kuwaasa na kuwasihi wanafunzi wao wa kitaabiina juu ya uzito wa suala la deni na dhima yake.

Huyu hapa Swahaba Abdullaah  bin ‘Umar (ALLAAH Awaridhi!) , anamwambia Humraan (Allaah amraham!):

“Ewe Humraan! Muogope ALLAAH, na wala usife ilhali wadaiwa kwani yatakwenda kuchukuliwa mema yako, na siku hiyo hakuna kulipana kwa diinaar wala kwa dirham”.  Musannaf wa Abdurrazzaaq 3/57.

Pamoja ya kuwa imeswihi hadithi kutoka kwa Mtume (swalla LLAAHU ‘alayhi wasallam) kwamba:

“Yeyote atakayekufa na deni la mali za watu, hali yakuwa ana nia ya kuzilipa basi ALLAAH atamlipia”.

Hili ni kwa yule ambaye hakuacha mali ambayo ingetumika kuziba pengo la deni la watu, au  mawalii wake hawakulijua deni hilo na yeye hakupanga kumdhulumu mdai wake ila tu mauti yalizuia baina ya kulipa deni hilo.

Na kwa uzito wa suala la deni, Mtume (swalla LLAAHU ‘alayhi wasallam) ametufunza dua ya kumuomba ALLAH atusahalishie uzito wa kulip madeni ya watu.

اللهم اكفني بحلالك عن حرامك, واغنني بفضلك عمن سواك

“Ewe ALLAAH!  nitosheleze mimi kwa halali yako kutokamana na uliyoyaharamisha,  na nipe utajiri kwa fadhla zako kutokana na asiyekuwa wewe!”.   Tirmidhiy na ameihasanisha Al-Imaam Al-Albaaniy (ALLAAH Amraham!).

اللهم استر عورتي وآمن روعتي واقض عني ديني” الطبراني في الكبير.

“Ewe ALLAAH! Nisitiri kwa aibu zangu, na unipe amani kwa ninayoyachelea, na unilipie madeni yangu”. Al-Twabaraaniy.

والله ولي التوفيق.