Radd Yenye Nguvu Kwa Hajaawirah Na Wenye Kusema Adhaana Ya ´Uthmaan Ni Bid´ah 4


Adhaana ya pili siku ya Ijumaa ni Sunnah. Hili halina shaka yoyote. Sijui yeyote mwenye kuonelea kinyume.

 

Kuhusu adhaana ya kwanza iliyopo kabla ya adhaana ya hii – adhaana ya pili – ilisuniwa na kiongozi wa waumini ´Uthmaan (Radhiya Allaahu ´anh). Sunnah ya kiongozi mwongofu ni yenye kufuatwa. Kwa kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

 

“Jilazimieni na Sunnah zangu na Sunnah za makhaliyfah wangu waongofu baada yangu. Shikamaneni nazo barabara na ziumeni kwa magego yenu.”

 

Endapo mtu atauliza ni vipi tutatendea kazi hili ilihali Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakulitendea kazi. Nitamjibu kwamba tutalitendea kazi kwa kuwa haya ni katika mambo ya Ijtihaad ya yule ambaye Sunnah yake inastahiki kufuatwa. Naye si mwengine ni kiongozi wa waumini ´Uthmaan bin ´Affaan (Radhiya Allaahu ´anh). Ieleweke kuwa hakuna Sunnah yoyote kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) inayoenda kinyume nayo. Sababu iliyopelekea kuweka adhaana hii wakati wa ´Uthmaan haikuwepo wakati wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

 

Imethibiti kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ya kwamba Bilaal katika Ramadhaan anaadhini kabla ya Fajr kuingia. Lengo sio kwa sababu Fajr imeshaingia, lengo ni kwa sababu ya kumuamsha mwenye kulala na kumzindua aliye macho. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

 

“Hakika Bilaal anaadhini usiku ili kumzindua aliye macho na kumuamsha mwenye kulala. Hivyo, kuleni na kunyweni mpaka msikie adhaana ya Ibn Umm Maktum. Kwani hakika yeye haadhini mpaka Fajr iingie.”

 

Kwa kifupi ni kwamba adhaana ya pili siku ya Ijumaa haina utata wala mashaka yoyote. Isitoshe ilikuwepo wakati wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

 

Ama kuhusu adhaana ya kwanza ni katika Sunnah za ´Uthmaan (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye ni mmoja katika makhaliyfah waongofu ambao wana Sunnah inayostahiki kufuatwa.

 

Mzungumzaji: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn

Chanzo: https://www.youtube.com/watch?v=zPQKZmXrL8s

Toleo la: 15.11.2015

Imefasiriwa na: Wanachuoni.com