Radd Yenye Nguvu Kwa Hajaawirah Na Wenye Kusema Adhaana Ya ´Uthmaan Ni Bid´ah 5


Endapo mtu atasema kuwa kuzua hilo – yaani adhaana ya kwanza ya Ijumaa – ni Bid´ah kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakuweka isipokuwa tu adhaana moja. Adhaana ni ´ibaadah na haiwezi kuwekwa isipokuwa kwa kuwepo idhini kutoka katika Shari´ah. Tutamraddi kwa njia mbili:

 

Ya kwanza: Hii ni Sunnah ya makhaliyfah waongofu ambapo ´Uthmaan (Radhiya Allaahu ´anh) ni mmoja katika wao. Makhaliyfah waongofu wana Sunnah yenye kustahiki kufuatwa. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

 

“Jilazimieni na Sunnah zangu na Sunnah za makhaliyfah wangu waongofu baada yangu.”

 

Ya pili: ´Uthmaan (Radhiya Allaahu ´anh) aliiweka kwa sababu ambayo haikuwepo wakati wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Sababu yenyewe ni kupanuka kwa al-Madiynah na watu kuzidi kuwa wengi. Sababu ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kutoiweka katika wakati wake ni kwa kuwa wakati wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) mji ulikuwa haujapanuka na hivyo watu hawakuwa na haja nayo.

 

Kama inavyojulikana ni kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakuweka adhaana mwishoni mwa usiku kwa sababu muda wa swalah ya Fajr umeshaingia. Sababu ilikuwa ni kumuamsha mwenye kulala na kumzindua aliye macho. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

 

“Bilaal anaadhini usiku ili kumuamsha aliye lala na kumzindua aliye macho. Hivyo kuleni na kunyweni mpaka msikie adhaana ya Ibn Umm Maktum. Hakika yeye haadhini mpaka Fajr iingie.”

 

Kwa hivyo sababu iliyompelekea Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuadhiniwe mwishoni mwa usiku haikuwa kwa sababu muda wa swalah umeshaingia, bali ilikuwa ni kwa sababu ya kuwaandaa watu wapate daku. Hii angalau inaweza kuwa ni sababu ndogo ya uwekwaji wa adhaana ya kwanza siku ya Ijumaa. Kujengea juu ya haya hii inakuwa ni Sunnah iliyosuniwa na kiongozi wa waumini ´Uthmaan bin ´Affaan (Radhiya Allaahu ´anh). Hivyo ni Sunnah ya Kishari´ah ambayo sisi tumeamrishwa kuifuata.

 

Kutokana na haya inapata kujulikana jeuri ya baadhi ya wanafunzi wachanga ambao wanajinasibisha na elimu ya Hadiyth kwa kitendo chao cha kumtia upotofuni kiongozi wa waumini ambaye ni ´Uthmaan bin ´Affaan (Radhiya Allaahu ´anh) na kusema kuwa ni mtu wa Bid´ah. Wakisema kuwa ´Uthmaan ni mtu wa Bid´ah basi hilo linalazimisha Maswahabah wote waliokuwepo wakati wake wao pia ni wazushi kwa kuwa walikubali Bid´ah! Mwenendo wa khatari kabisa ambao unatokamana na jeuri na mtu kujiona. Ninaapa tena na tena na tena ya kwamba elimu ya as-Salaf as-Swaalih iko karibu na usawa na uongofu zaidi kuliko elimu ya waliokuja nyuma. Hili ni jambo linalojulikana fika…

 

Mimi ninawatahadharisha ndugu zangu wanafunzi kushika msimamo kama huu khatari. Ninawaambieni: tahadharini kushika misimamo ya khatari. Lazimianeni na Sunnah za makhaliyfah waongofu, kama alivyokuamrisheni Mtume wenu (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Tahadharini na kuziachia ndimi zenu dhidi yao kwa maneno kama haya ya kipumbavu. Hivi kweli mtu anaweza kuthubutu kusema kuwa ´Uthmaan bin ´Affaan (Radhiya Allaahu ´anh) – ambaye ni kiongozi wa tatu katika Uislamu – au Maswahabah waliokuwepo katika zama zake ya kwamba ni wazushi na waliitikia Bid´ah? Wewe ni nani [mtoto] mchanga! Wewe ni nani ulodanganywa!

 

Mzungumzaji: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn

Chanzo: https://www.youtube.com/watch?v=_zSYlxVIKys

Toleo la: 16.01.2016

Imefasiriwa na: Wanachuoni.com