Radd Yenye Nguvu Kwa Hajaawirah Na Wenye Kusema Adhaana Ya ´Uthmaan Ni Bid´ah 6


Asli ni kuwa Ijumaa ina adhaana moja. Nayo inakuwa pale imamu anapoingia [msikitini]. Hali ilikuwa namna hii wakati wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Ilikuwa pindi Khatwiyb anapoingia ndio Bilaal (Radhiya Allaahu ´anh) anaadhini. Halafu ndipo ´Uthmaan (Radhiya Allaahu ´anh) akazidisha adhaana ya pili, jambo ambalo limependekezwa. Lengo ilikuwa kuwazindua watu ya kwamba ni siku ya Ijumaa. Adhaana hii inatolewa kabla ya ile adhaana ya pili pindi imamu anapoingia. Kunaadhiniwa nusu saa, saa moja n.k. kabla ya kuingia wakati ili watu wajue kuwa ni Ijumaa na wajiandae kuja. Salaf waliendelea katika hali hii hali ya kumuiga ´Uthmaan (Radhiya Allaahu ´anh) tangu wakati wa ´Uthmaan, ´Aliy na wakati wa Maswahabah baada ya ´Uthmaan. Hili ni jambo limewekwa katika Shari´ah tokea wakati wa makhaliyfah waongofu. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

 

“Jilazimieni na Sunnah zangu na Sunnah za makhaliyfah wangu waongofu baada yangu.”

 

Ni jambo linalojulikana vyema kuwa ´Uthmaan na ´Aliy (Radhiya Allaahu ´anhumaa) wote ni katika makhaliyfah waongofu.

 

Sunnah ni kuwa inatakiwa kutoa adhaana ya kwanza siku ya Ijumaa kwa lengo la kuzindua, kama alivyofanya ´Uthmaan (Radhiya Allaahu ´anh) na waliokuja baada yake.

 

Swali 2: Kuna wenye kuonelea kuwa adhaana ya kwanza siku ya Ijumaa sio katika Sunnah kwa kuwa haikuthibiti kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kujengea juu ya hili wanaonelea kuwa ni wajibu kuachana na jambo hili. Upande mwingine kuna wenye kuonelea kuendelea na adhaana hii ya kwanza. Ni upi mtazamo wako?

 

Jibu: Adhaana ya kwanza ni katika Sunnah kwa kuwa ilifanywa na ´Uthmaan (Radhiya Allaahu ´anh) na ´Aliy na Maswahabah wengine wakamkubalia hilo. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

 

“Jilazimieni na Sunnah zangu na Sunnah za makhaliyfah wangu waongofu baada yangu.”

 

´Uthmaan na ´Aliy (Radhiya Allaahu ´anhumaa) ni katika makhaliyfah waongofu. Ni jambo lilifanywa na ´Uthmaan na ´Aliy na Maswahabah wengine wakamkubalia hilo. Adhaana hii ina faida. Lengo lake ni kuwazindua watu ya kwamba ni siku ya Ijumaa ili waweze kujiandaa kwenda [msikitini]. Sio Bid´ah. Uhakika wa mambo ni Sunnah kwa sababu ni katika Sunnah za makhaliyfah waongofu. Kwani Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ndiye kausia hayo.

 

Mzungumzaji: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdil-´Aziyz bin Baaz

Chanzo: https://www.youtube.com/watch?v=txqXO7mzis8

Toleo la: 17.01.2016

Imefasiriwa na: Wanachuoni.com